Na Anna Nkinda – Kuala Lumpur, Malaysia
CHUO Kikuu cha Binary cha nchini Malaysia kimetoa nafasi 10 za ufadhili wa masomo ya shahada ya Uzamili na Uzamivu katika fani za Ujasiriamali na Teknolojia ya Habari kwa kipindi cha miaka mitatu kwa Watanzania wataohitaji kusoma nchini humo.
Utiaji saini wa makubaliano ya nafasi hizo za masomo zinazojulikana kwa jina la Binary – First Lady of Tanzania Scholarship Award umefanyika leo katika chuo hicho kati ya Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), Daud Nasibu na Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph Adaikalam na kushuhudiwa na Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utiaji saini Mke wa Rais Mhe. Mama Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA alikishukuru chuo hicho kwa kutoa nafasi 10 za masomo ambazo zitasaidia sio tu kwa wataofaidika nazo moja kwa moja bali pia kwa jamii ambako wahitimu watarejea kuitumikia.
Mama Kikwete alisema kupitia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now) kwa upande wa elimu ya msingi na sekondari Tanzania imelenga kujenga uwezo wa walimu kwa kutoa mafunzo ya pahala pa kazi, kusaidia watoto wasiofanya vizuri kwa kuandaa vitendea kazi mahsusi vinavyozingatia umri na mahitaji, kuboresha miundo mbinu kwa kujenga madarasa, maabara na nyumba za walimu, kuboresha vifaa vya ufundishaji kama vile madawati, vifaa vya maabara, vitendanishi (Kemikali) na uongeza motisha kwa walimu.
“Mipango niliyotaja hapo juu imekuwa na mafanikio makubwa kuongeza maradufu udahili wa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari, kuleta usawa wa kijinsia na kupunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa walimu, maabara, vitabu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia”.
Kwa mukhtadha huo ni dhahiri kwamba fursa za Binary First Lady of Tanzania Scholarship zimekuja kwa wakati muafaka kabisa ambapo shule zetu za sekondari na taasisi za elimu ya juu zinatoa wahitimu wengi wanaohitaji kupata elimu za ngazi za juu za shahada za uzamili na uzamivu. Hivyo basi narudia kuwashukuru kwa moyo wenu wa upendo na ukarimu. Mmeifanyia nchi yetu ihsani kubwa,” alisema Mama Kikwete.
Naye Mwanzilishi na Mwenyekiti Mtendaji wa chuo hicho Prof. Joseph Adaikalam alisema nia ya ufadhili huo wa masomo ni kutoa nafasi kwa wanafunzi Watanzania kupata ujuzi na utaalamu maalum ili watakapomaliza masomo na kurudi nyumbani waweze kuchangia katika maendeleo ya nchi na kuwasaidia moja kwa moja watanzania.
“Binary – First Lady Scholarships ambayo iko chini ya mwamvuli wa Binary Global Scholarship Fund ilianzishwa mwaka 2009 hadi sasa nafasi hizo za masomo zimeshatolewa katika nchi za Zambia, Kenya na Senegali”.
Pia chuo kinatoa ufadhili wa masomo kwa nchi ambazo hazina mke wa Rais ufadhili unaojulikana kwa jina la Binary Malaysia – Bosnia Herzegovina, na Binary Malaysian – Uzbekistan hii yote ni kuonyesha kuwa vyuo vikuu vya Malaysia vinatambua umuhimu wa elimu”, Prof. Adaikalam.
Alisema wanafunzi wataoomba ufadhili huo wa masomo kwa shahada ya Uzamili kiwango chao cha ufaulu kitaanzia CGPA ya 3.5 na kuendelea na watakaokidhi vigezo wataanza masomo mwezi wa 10 mwaka huu nchini humo.
Taasisi ya WAMA ni msimamizi wa Binary – First Lady of Tanzania Scholarship utakaotolewa kwa kipindi cha miaka mitatu na baada ya hapo utasainiwa tena kwa kipindi kama hicho na kwa mwaka huu nafasi zitatolewa kwa wanafunzi wa masomo ya Uzamili. Mwakani ufadhili utatolewa kwa wanafunzi wa Shahada ya Uzamili na Uzamivu.