MAMLAKA ya Elimu na mafunzo ya Ufundi stadi (VETA) kupitia chuo cha VETA Mikumi inatarajia kuanzisha kozi ya utalii wa kitamaduni ili kuwafundisha watanzania tamaduni, mila na desturi ili kuulinda utamaduni wetu, ambao unaonekana kupotea kadri teknolojia inavyozidi kukua kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari walipotemebelea chuo hicho Cha VETA Mikumi, Mkuu wa chuo hicho Christopher Ayo amesema kuwa uamuzi huo umetokana na sekta ya utalii kuendelea kukua mwaka hadi mwaka huku jamii ikionekana kusahahu uhasilia wa tamaduni mbalimbali za kitanzania.
Amesema utamaduni ukitumika ipasavyo unaweza kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii pamoja na uchumi nchini kutokana na ukweli kwamba nchi nyingi duniani zimeweza kulinda utamaduni kuweza kukuza uchumi wao.
Amesema chuo chake kwa kushirikiana na Chuo cha NOVA Scotia Communinity College cha nchini Canada kinaanda kozi hiyo itakayowezesha watanzania kujifunza kwa undani kuhusu utamaduni wao kama vile ngoma, vyakula vya asili, sanaaa na historia ya makabila mbalimbali. Ayo amesema maandalizi ya kuanzisha kozi hiyo yapo kwenye hatua za mwisho na kwamba kuanzia Januari, 2017 masomo yataanza kutolewa.
Aidha mkuu huyo amesema walimu watano watakaofundisha masomo hayo wameshaandaliwa na kupatiwa mafunzo nchini Canada jinsi ya kutumia technologia katika kufundisha na kuandaa mitaala. Ayo amesema VETA Mikumi itaendelea kutoa mafunzo kwa jamii inayowazunguka katika kuwaandaa vijana katika soko la ajira kwa kujiajiri au kuajiriwa na kuweza kuendesha maisha yao na kuchangia pato la taifa.
Ametoa rai kwa vijana wa mikumi na maeneo ya mengine ya Mkoa wa Morogoro kuchangamkia fursa za mafunzo zilizopo chuoni hapo ili kuweza kuwa sehemu ya wataalam watakaohudumia viwanda vitakavyojengwa kutokana na serikali ya awamu ya tano ya Rais Dk. John Pombe Magufuli kuweka msisitizo wa kuhakikisha nchi inakuwa ya viwanda.