Na Mwandishi Wetu
MSANII nyota wa dansi nchini Tanzania, Christian Bella pamoja na Vanessa Mdee wa miondoko ya bongo fleva wanatarajia kutumbuiza katika mjadala wa wazi utakaofanyika Desemba 3, 2014 ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za maadhimisho ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi wa TGNP Mtandao Lilian Liundi, onesho hilo litafanyika sambamba na mjadala wa wazi kujadili na kuwezesha uelewa juu ya umuhimu wa mgawanyo wa rasilimali katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuboresha afya ya jamii na kuondokana na madhara yatokanayo na tohara kwa wanawake na mimba za utotoni.
Bi. Liundi alisema mjadala huo utakao anza saa 3 asubuhi katika viwanja vya TGNP Mtandao, Mabibo Dar es salaam, pia utatoa nafasi kwa washiriki kuonesha mafanikio, kutoa shuhuda na kueleza changamoto wanazokumbana nazo katika kupambana na ukatili wa kijinsia na hivyo kujiimarisha katika kukabiliana na changamoto hizo.
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi huyo, imeeleza kuwa mgeni rasmi katika mjadala huo anatarajia kuwa Katibu Mjendaji wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania Bi. Mary Massey.
“…Malengo ya mjadala huo ni kujadili na kuwezesha uelewa juu ya umuhimu wa mgawanyo wa rasilimali katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuboresha afya ya jamii na kuondokana na madhara yatokanayo na tohara kwa wanawake na mimba za utotoni,” ilifafanua taarifa hiyo.
Mjadala huo pia ni nafasi kwa washiriki kuonesha mafanikio, kutoa shuhuda na kueleza changamoto wanazokumbana nazo katika kupambana na ukatili wa kijinsia na hivyo kujiimarisha katika kukabiliana na changamoto hizo.
Aidha kauli mbiu itakayoongoza mjadala huo ni “Siyumbishwi, Najilinda, Mnilinde” unaojikita kwa vijana hasa wa kike ikiwahimiza wasiyumbishwe, wajiepushe au wajilinde na mambo au mazingira hatarishi na kuitaka jamii iwajibike kuwalinda na kuwakinga vijana dhidi ya ukatili wa kijnsia unaotokea katika mazingira mbalimbali katika nchi yetu.