CHODAWU yavunja Kamati ya Utendaji ya Taifa

Na Anna Titus na Esther Muze, Maelezo-Dar es Salaam,

BARAZA Kuu Maaluum la Chama cha Wafanyakazi wa Hifadhi, Mahoteli, Majumbani na kazi nyingine (CHODAWU) limevunja Kamati ya Utendaji ya Taifa iliyokuwepo na kutengua uteuzi wa aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu, Kiwanga Towegale.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa Idara ya Habari (MAELEZO) jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa Kikao cha Baraza Kuu maalum, Paul Msilu imesema licha ya kutengua nafasi ya Katibu Mkuu CHODAWU, baraza hilo pia limeondoa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu iliyokuwa ikishikiliwa na Francis Maembe.

Aidha Baraza hilo limechagua Kamati mpya ya Utendaji ya Taifa itakayosimamia shughuli za uendeshaji kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu ambayo itaongozwa na Said Wamba.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, Wamba ataiongoza Kamati mpya ya utendaji ya Taifa katika kipindi cha mpito cha Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mapema mwanzoni mwa mwezi Septemba 2011.

Pia Baraza Kuu limeomba wanachama na wadau wote kutoa ushirikiano kwa Kamati hiyo mpya katika kutekeleza jukumu la kuratibu shughuli zote za uchaguzi.

Maamuzi ya Baraza hilo yamefanyika katika ukumbi wa hoteli ya Mbezi Garden Jijini Dar es Salaam tarehe 3,Agosti 2008