CHIPUKIZI CUP KUANZA DISEMBA 11.

FKB_7697Michuano ya vijana ya Nchi za Afrika Mashariki kwa Mpira wa miguu, yajulikanayo kama “ Chipukizi Cup” yanatarajiwa kuanza kuchezwa Disemba 11 hadi 13 yakishirikisha vijana walio na umri wa miaka 10 hadi 18 kutoka ndani na nje ya nchi.

Zaidi ya vijana 300 watashiriki kuchuana vikali katika mashindano hayo ya siku tatu yatakayofanyika katika viwanja vya shule ya Kimataifa ya Moshi tawi la Arusha (ISM).

Mkurugenzi wa Taasisi ya kuinua na kukuza vipaji kwa vijana (Future stars academy) ambao ndio waandaaji, Alfred Itael alieleza kuwa mashindano hayo hufanyika kila mwaka jijini hapa yakiwa na lengo la kuwakutanisha vijana ,kuinua na kukuza vipaji vyao katika soka vile vile yanasaidia kujenga mahusiano mazuri ya michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“ Mpaka sasa Tayari timu 28 kutoka nchi za Kenya,Uganda,Burundi na wenyeji Tanzania Zimesibitisha kushiriki na tunategemea kupata timu nyingi zaidi” alisema Itaeli.

Itaeli alizitaja baadhi ya timu zitakazokuwa katika mashindano hayo kuwa ni pamoja na Ligi ndogo academy- Kenya,Express academy –Uganda, Young life academy,small nyota pamoja na wenyeji Future stars academy za Arusha pamoja na timu nyinginezo.

“Mashindano haya kwa vijana yatasaidia kuwajengea uwezo mkubwa vijana pia kuwa na ujuzi katika soka pamoja na kujiamini kwani tukifanya hivi kuanzia ngazi za watoto tutafika mbali kimichezo kama ilivyo kwa nchi mbalimbali zilizoendelea kimichezo”aliongeza Itaeli.

Mashindano hayo yanaendeshwa kwa mfumo wa mtoano katika makundi baadae robo fainali,nusu fainali na fainali ambapo washindi watakabidhiwa zawadi.

Taasisi ya kukuza vipaji kwa vijana ya Future stars Academy ndio waandaaji wa mashindano hayo ikiwa ni mara ya tano sasa kufanyika tangu yaanzishwe rasmi mwaka 2011.