China Yatoa Mabilioni ya Fedha Kuwekeza Miradi Anuai Tanzania

*Maendeleo ya China ni Cachu….!
TANZANIA na Jamhuri ya Watu wa China Oktoba 23, 2014, zimetiliana saini Hati za Makubaliano (Memorandum of Undestanding) ambako taasisi za China zitawekeza mabilioni ya dola za Marekani katika uchumi wa Tanzania. Shughuli hiyo ya utiaji saini imekuwa sehemu ya Mkutano wa Tatu wa Uwekezaji Kati ya Tanzania na China uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Nyumba ya Kufikia Wageni wa Serikali ya Diaoyutai mjini Beijing, China.

Aidha, utiaji saini huo ambao utaziwezesha taasisi kadhaa za Tanzania kunufaika na mitaji na uwekezaji kutoka China ulikuwa sehemu ya ziara rasmi ya Kiserikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika China kwa mwaliko wa Rais Xi Jinping. Rais Kikwete ameshuhudia shughuli hiyo ya utiaji saini.

Miongoni mwa Makubaliano yaliyotiwa saini ni pamoja na Makubaliano ya Ushirikiano wa Kimkakati kati ya Shirika la Nyumba Tanzania (NHC) na Kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (CRJE) ambako kiasi cha dola bilioni moja unusu zitawekezwa katika uchumi wa Tanzania.

Kiasi cha dola bilioni moja zitawekezwa katika ujenzi wa mji mpya wa Salama Creek Satellite, eneo la Uvumba, Wilaya yaTemeke, Dar es Salaam na kiasi cha dola milioni 500 zitawekezwa katika ujenzi wa Financial Square, eneo la Upanga. Aidha, NHC itapata kiasi cha dola za Marekani milioni 200 kutoka Kampuni ya Poly Technologies kwa ajili ya ujenzi wa Mradi wa Valhalla, eneo la Masaki, Dar es Salaam.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limetiliana saini Makubaliano na Kampuni ya Hengyang Transformer ambako Kampuni hiyo ya Tanzania itapata mamilioni ya dola za Marekani kwa ajili ta mradi wa kusambaza umeme vijijini.
Aidha, Shirika hilo la TANESCO limetiliana saini Makubaliano ya ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Kinyerezi IV.

Halmashauri ya Manispaaa ya Temeke, Dar es Salaam imetiliana saini Makubaliano na Kampuni ya Jiangyin Tianhe Gasses Group ya ujenzi wa barabara ya lami ya Kikwete Friendship Highway katika Wilaya ya Temeke. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Saidi Mecky Sadiq na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mheshimiwa Sofia Mjema wameshuhudia utiaji saini Makubaliano hayo.

Vile vile, Mkoa wa Pwani, umetiliana saini Makubaliano na Kampuni ya Jiansu Shenli Plastics Gropu Limited ya China kwa ajili ya kugharimia na kuendeleza Mradi wa Viwanda na Uchumi katika eneo la Mlandizi. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mama Mwantumu Bakari Mahiza ametia saini kwa niaba ya Mkoa wake.

Wakati huo huo; RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa maendeleo ya haraka ya Jamhuri ya Watu wa China ni hamasa kubwa na ya kutosha kwa nchi za Afrika kuwa nazo zinaweza kuendelea katika kipindi kifupi kama zitaongozwa na sera sahihi za mageuzi ya kiuchumi.
Rais Kikwete ameyasema hayo Oktoba 24, 2014, wakati alipokutana kwa mazungumzo rasmi na Mwenyekiti (Spika) wa Bunge la Jamhuri ya Watu wa China, National People’s Congress (NPC) Mheshimiwa Zhang Dejiang, ikiwa ni moja ya shughuli za Mheshimiwa Rais katika ziara yake rasmi ya China.
Katika mazungumzo hayo kwenye Jengo la Bunge la Great Hall of the People mjini Beijing, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Dejiang: “China inatuhamasisha sana kwamba na sisi tunaweza kupata mabadiliko na maendeleo ya haraka ya wananchi wetu ili mradi tu tuweze kuwa na sera sahihi ambazo zinalenga katika kuleta mageuzi ya msingi na ya kweli kweli ya kiuchumi”.
Rais Kikwete amesema kuwa kwake yeye ambaye amekuwa anatembelea China kila baada ya wastani wa miaka minne, mabadiliko ya China yanatia hamasa kweli kweli kuwa nchi za Afrika pia zinaweza kuleta mageuzi makubwa ya maisha ya watu wake.
“Nilikuja hapa kwa mara ya kwanza mwaka 1980, na tokea wakati huo nimetembelea nchi hii kila baada ya miaka minne kwa wastani na kila nikija nashuhudia mabadiliko makubwa yasiyopimika na wala kufikirika. China ilikuwa nchi masikini sana wakati nilipofika hapa kwa mara ya kwanza lakini katika miaka 30 tu imebadilika kutoka nchi masikini na kuwa nchi iliyoendelea na yenye uchumi unaoshikilia nafasi ya pili kwa ukubwa duniani,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Tunawapongeza sana kwa juhudi ambazo zimewafikisheni hapa. Mnatuhamasisha na sisi kuwa ipo siku moja na sisi katika Afrika tutafikia hatua hii ya maendeleo.”
Naye Mheshimiwa Dejiang amemkubusha Rais Kikwete mazungumzo kati yao wakati walipokutana kwa mara ya kwanza miaka saba iliyopita Ikulu, mjini Dar es Salaam. Wakati huo, Mheshimiwa Dejiang alikuwa Katibu wa Chama Tawala cha Kikomunisti cha China katika Jimbo la Guangzhou, jimbo ambalo linaongoza katika China kwa kufanya biashara na Tanzania. Kati ya biashara zote ambazo Tanzania na China zinafanya, asilimia 60 inatokea Jimbo la Guangzhou.
Dejiang pia amepongeza mahusiano mazuri kati ya Tanzania na China katika miaka 50 tokea nchi hizo mbili kuanzisha uhusiano wa kibalozi Aprili 26, mwaka 1964.
Mwenyekiti huyo wa Bunge pia amesema kuwa ujenzi wa Reli ya TAZARA unaendelea kuthibitisha urafiki baina ya watu wa China, Tanzania na Zambia na kuongeza kwa Tanzania kwa kuimarisha TAZARA na kwa kutilia maanani utajiri na raslimali zilizopo, ikiwemo nafasi ya kijiografia, utulivu na amani na idadi kubwa ya watu, Tanzania ina sifa ya kuwa nchi tajiri katika miaka isiyokuwa mingi ijayo.