China Yaendelea Kukuza Ushirikiano na Tanzania

Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini, Lu Younqing (Kushoto) alipokutana na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Pombe Magufuli (katikati) katika Ofisi za Makao Makuu ya Wizara ya Ujenzi, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Balozi Herbert E. Mrango.

JAMHURI ya Watu wa China imeendelea kuonesha dhamira yake ya kukuza ushirikiano na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan katika sekta ya ujenzi. Hali hiyo imejiri baada ya Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China hapa nchini, Lu Younqing kufanya mazunumzo na Waziri wa Ujenzi Dk. John Pombe Magufuli alipomtembelea ofisini kwake na kubainisha azma hiyo ya kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo katika miradi ya maendeleo.

Miradi mingi mikubwa ya ujenzi hapa nchini imekuwa ikitekelezwa na makandarasi kutoka China. Makampuni hayo yamejikita zaidi katika maeneo ya ujenzi wa barabara, majengo makubwa, miradi ya maji, kilimo pamoja na miundombinu ya mawasiliano.

Waziri wa Ujenzi akimshukuru Balozi huyo kwa kumtembelea, amezipongeza kampuni za Kichina ambazo zinatekeleza miradi ya ujenzi wa barabara, madaraja na majengo hapa nchhini kwa kuzitekeleza kazi hizo kwa ubora unaoendana na viwango vilivyowekwa lakini kwa gharama nafuu.

Hata hivyo, Waziri Magufuli aliezea kuwepo kwa baadhi ya kampuni za Kichina ambazo utendaji wake hauridhishi kwamba Wizara yake haitasita kuzichukulia hatua kali za kisheria na amemuomba Mheshimiwa Balozi Younqing kushirikiana naye katika kuwafuatilia makandarasi wote watakaoanza kulichafua jina zuri ambalo linaendelea kujengaka kwa makampuni ya ujenzi kutoka China.

Naye, Balozi Younqing akimhakikishia ushirikiano Waziri wa Ujenzi, pia amemuarifu kwamba tayari maelekezo yametolewa kwa makandarasi wote wa Kichina wanaofanya shughuli zao hapa Tanzania kuhakikisha kuwa pale inapowezekana wanatumia bidhaa na mali ghafi zinazopatikana hapa nchini ikiwa ni pamoja na Wataalamu wa Kizalendo.