China Kupeleka Dola Milioni 85 Kusaidia Mapambano ya Ebola

Rais wa China, XI Jinping

Rais wa China, XI Jinping


JAMHURI ya Watu wa China Oktoba 24, 2014 imetangaza kuwa kwa mara ya nne katika kipindi kifupi inapeleka msaada wa dawa, vifaa na mahitaji mengine ya tiba yenye thamani ya dola za Marekani milioni 85 kukabiliana na ugonjwa wa Ebola kwa nchi tatu za Afrika Magharibi ambazo zinapambana na ugonjwa huo ambao mpaka sasa umeua zaidi ya watu 4,000.
Aidha, China imetangaza kuwa itajenga kituo kikubwa cha afya na tiba katika nchi ya Liberia kama sehemu ya kukabiliana na ugonjwa huo. Msaada huo mwingine wa China umetangazwa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, XI Jinping katika mazungumzo yake rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika kwenye The Great Hall of the People mjini Beijing ikiwa ni sehemu ya ziara rasmi ya Rais Kikwete, Rais Jinping amesema: “Hali katika Afrika sasa ni ya utulivu lakini yapo matishio ya mara kwa mara mengine ya ndani ya Afrika na mengine ya nje na mojawapo ya matishio hayo ni ugonjwa wa Ebola.”
Ameongeza Rais Jinping: “Mpaka sasa, Jamhuri ya Watu wa China imetuma misaada ya dawa na raslimali nyingine mara tatu kwa nchi tatu za Afrika Magharibi ambazo zinakabiliana na ugonjwa wa Ebola. Napenda kutangaza leo kuwa China, kwa mara nyingine, imeamua kupeleka msaada mwingine wenye thamani ya RMB 500 ikiwa ni fedha taslim, wataalam wa afya,wataalam wengine na raslimali nyingine.”
Ameongeza Rais Jinping: “China pia itajenga kituo kikubwa cha afya na tiba ili kiweze kusaidia nchi zote tatu ambazo zinakumbwa na ugonjwa huo wa Ebola Liberia, Guinea na Sierra Leone. Tunaungana na wananchi wa nchi hizo tatu katika kubaliana na tishio hili kubwa ambalo kwa hakika linahitaji ushirikiano wa dunia nzima.”
Rais Kikwete ambaye anaendelea na ziara yake katika China mapema leo amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la China la National People’s Congress, Zhang Deajing. Aidha, Rais Kikwete amekutana kwa mazungumzo na Waziri Mkuu wa China, Li Keqiang.