Chenge Aanza ‘Kumwaga’ Bilioni za Escrow Bariadi

Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge

Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge

MBUNGE wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge sasa ni kama ameanza kurudisha Shilingi bilioni 1.6 fedha alizopewa kama mgao zilizochotwa katika kaunti ya Tegeta Esrow baana ya jana kuongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa maabara Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ambapo amechangia milioni 116 kati ya shilingi milioni 174.06 zilizopatikana katika harambee hiyo.
  
Mbunge huyo ambaye alitajwa kupewa fedha kiasi cha bilioni 1.6 katika kashfa ya uchotwaji wa fedha akaunti ya Tegeta Esrow, alichangia kiasi hicho huku akikwepa kuongelea kashfa hiyo inayomkabili.

Harambee hiyo ambayo ilikuwa imeandaliwa na Halmashauri ya Mji wa Bariadi, ilikuwa na lengo la kukusanya fedha kiasi cha shilingi milioni 400, fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa maabara wilayani hapa.

Hata hivyo mbunge huyo alisema kuwa katika mchango wake, milioni 115 zitatumika kununua bati 500 ambazo alisema ameamua kuezeka maabara zote ambazo zimekamilika ujenzi wake na ambazo hazijakamilika kwa wilaya nzima. Kuhusu kupokea fedha bilioni 1.6, kutoka katika akaunti ya Tegeta Esrow, mbunge huyo hakuweza kuzumgumzia kashfa hiyo na kubaki akitoa misemo kwa lugha ya kisukuma.

“…suala la Escrow tuachane nalo kuna sehemu husika katika majukwaa nitaliongelea na wananchi wangu…hapa tuzumgumzie elimu na arambee hii…hilo tuliache uko Dodoma na siyo la hapa Bariadi,” alisema Chenge

Akiongea alisema “tuache hayo ya Dodoma mimi ndiye nyoka mwenye makengeza” neno aliloliongea kwa lugha ya kisukuma “Nene Nale nzoka ihenge” na kuongezeka kuwa yeye ni tumbili “Nene nale nhombele.

Baadhi ya washiriki katika arambee hiyo walieleza kuwa mbunge huyo alikuwa akimaanisha kuwa yeye anajua mengi sana kuliko wengine wanavyodhani na amepata bahati ambayo wengine hawawezi kuipata.

Wengine walieleza kuwa maneno ya mbunge huyo yalikuwa na maana kubwa, ambapo walibainisha kuwa alieleza kuwa kuna watu wengine wanajifanya wao wanafahamu kila kitu hapa nchini, wakiwa hawajui kuwa kuna watu waliwatangulia kujua.
*Chanzo: Wanabidii