Na Zawadi Msalla
CHAMA Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA) kimesikitishwa na kitendo cha ushiriki mbovu wa Viziwi katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba kote nchini.
Akizungumza na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Habari-MAELEZO leo, Mshauri Mwelekezi wa Elimu ya Uraia kwa Watu wenye Ulemavu, Bw. Novat Rukwago alisema kuwa, licha ya jitihada mbalimbali ambazo walijaribu kuzifanya ili kuhakikisha viziwi kote nchini wanapata haki yao ya msingi na ya kikatiba ya kupiga kura bado ushiriki wao haukuridhisha.
Rukwago alizitaja changamoto mbalimbali zilizo jitokeza katika uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na ukosefu wa wataalamu wa lugha za alama zinazotumiwa na viziwi katika kampeni mbalimbali za Vyama vya Siasa, hivyo sera na Ilani za vyama hivyo hazikuweza kujulikana kwa viziwi.
“Vyama vingi vilisema ni suala la rasilimali na ukosefu wa fedha za kuweka wataalamu hao, ingawa tuonavyo sisi ni kwamba walishindwa kutoa kipaumbele na si suala la fedha,” alisema Rukwago.
Aidha, Rukwago alisema CHAVITA kwa juhudi binafsi waliweza kutembea jumla ya mikoa 17 kote nchini na kufanikiwa kutoa elimu kwa baadhi ya viziwi ambapo jumla ya viziwi 2516 walijiandikisha, idadi hiyo ikiwa na wanaume 1256 na wanawake 1260. Waliopiga kura walikuwa ni 1807. Aliongeza kwa kusema kuwa licha ya changamoto hizo pia mazingira ya kupigia kura hayakuwa rafiki kwa watu wenye uhitaji maalumu kwani hakukuwa na wataalamu wa lugha za alama katika vituo vya kupigia kura.
Waliiomba Serikali kuzingatia umuhimu wa kuyapa kipaumbele makundi mbalimbali yenye uhitaji kwa chaguzi zijazo na kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kufanya mawasiliano na vyama vya watu wenye uhitaji maalum mapema ili kuweza kushirikiana katika kuondoa changamoto zilizojitokeza katika uchaguzi wa mwaka huu.