Muungano huo kwa mujibu wa CHAUMMA ni harakati za kuwakomboa watanzania kutoka mikononi mwa watu ambao wamejipa haki ya kutawala kwa hila na kila aina ya ulaghai kugeuza kuwa ndiyo ajira yao ya kudumu ili mradi waendelee kushikiria madaraka ya kuongoza nchi bila ya kujali maendeleo ya msingi kwa wananchi.
Mwenyekiti CHAUMMA taifa Mh. Hashim Rungwe anavipongeza vyama hivyo kwa jitihada zao za kuunganisha nguvu ya umoja ili kuwakomboa Watanzania kutoka katika makucha ya ugandamizwaji, hila, ubaguzi wa wananchi wengi kutoshirikishwa kutoa maamuzi ya uendeshaji wa nchi yao kwa zaidi ya miaka Hamsini.
Rungwe amewasifu viongozi hao kwa kuthubutu kwao kuwa mstari wa mbele kutetea na kuonesha njia sahihi inayoelekea kwenye Ukombozi wa raslimali zinazopotea ovyo kwa kudiriki kusema yaliyo dhahiri na kweli dhidi ya dola ya CCM.
Rungwe amesema makubaliano yao ni chachu ya kishujaa na ya walio wachache kuthubutu na kwamba CHAUMMA kipo nyuma yao na daima hakitasita kupaza sauti kwa umma kuwafungua macho watanzania kuanzia sasa kudai haki bila kukoma.
Rungwe amezidi kubainisha kuwa mapambano waliyoyaanzisha vyama vinne ni ya watanzania wote na anawashauri UKAWA waache mlango wazi kwa vyama vingine vyenye dhamira safi kujiunga nao katika kujenga na kuendeleza harakati hizi za kisiasa ili kupanua wigo wa kushiriki vyama vingine vya siasa kwa nia na moyo wa kizalendo.
Mwenyekiti huyo amewatahadharisha UKAWA kuwa macho na baadhi ya akina Eskarioti na Abu Jahl wasiopenda demokrasia ya uwajibikaji kwa vile katika msafara wa mamba na kenge wapo na wengine wemeanza kumlilia Mh. Rais hata kabla ya hukumu akiwataka wanaume kwa wanawake kukaza buti kwani faraja iko mbele yeo.
Rungwe amewataka Watanzania kuunga mkono jitihada za UKAWA bila kurudi nyuma kwa kuwa zina lengo la kumkomboa mnyonge na kumletea maisha salama endelevu dhidi ya utawala mbovu wa CCM na kwamaba kitendo cha chama tawala CCM na serikali yake kutupilia mbali maoni ya tume ya Jaji mstaafu Sinde Warioba ni dharau kwa Watanzania.
“Tusikubali na tunawaomba wananchi kwa ujumla msiikubali Katiba Inayopendekezwa na kuweni tayari kupiga kura ya hapana kwa kuwa haki yenu, mmepuuzwa na CCM,” Rungwe amesema. –
Amewapongeza pia wakazi wa jiji la Dar es Salaam kwa utayari wa kutumia muda wao vizuri kuhudhuria mkutano huo wa kihistoria na namna ya kipekee na kwamba wametumia raslimali zao vema kufanikisha makubaliano ya tukio hili muhimu linalokusudia kuwapa wananchi wengi elimu sahihi ya mfumo wa vyama vingi kwa siasa za nchi.
Pamoja na CHAUMMA kuibuka kidedea kwa kupata hati safi ya hesabu za serikali baada ya ukaguzi wa hesabu za chama kwa mwaka uliopita uliofanywa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa hesabu za serikali (CAG) .
Ni matumaini yetu kwamba vyama vingine vya siasa vitatoa ushirikiano kwa Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali na kujipatia hati safi kwani Chaumma kina amini Demokrasia ni pamoja na kuwa wasafi na wawazi kwenye mapato na matumizi ya chama.
Mh. Hashim Rungwe amelipongeza jeshi la polisi kwa kusimamia kusanyiko hilo bila ya kuwepo uvujifu wa amani na kuwaomba waendelee kujenga na kulinda misingi ya umoja huo kwani CHAUMMA kinaamini Mungu hatamwacha mja wake akae bure.
CHAUMMA Kinasisitiza kuwa tukio la jangwani lazima lilindwe kwa nguvu zote na kuwa macho na wachache watakao hatarisha umoja huu na UKAWA msisite kumuondoa ili lengo la kufanikisha ukombozi wa kweli ufikiwe na siasa za uvumilivu ni pale tu tunapoamini kuwa haki ipo na inatendeka sawa katika kudumisha demokrasia imara ilio sawia.
Source: East Africa TV (5EATV)