Taarifa inatolewa kwa umma kuhusu orodha ya wagombea waliorudisha fomu na utaratibu wa uchaguzi wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) ngazi ya taifa kama ifuatavyo
ORODHA YA WALIORUDISHA FOMU ZA KUGOMBEA: Nafasi ya Mwenyekiti (Wagombea 10)- Aidan Sadik P., Benard A. Mao, Benard Saanane, Deogratias Kisandu, Edwin Soko, Greyson Nyakarungu, Habib Mchange, John Heche, Masood S. Suleiman na Mtela Mwampamba. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Bara) (Wagombea 5) : Emanuel Somoin, Gwakisa B. Mwakasendo, Joseph Patric, Juliana Shonza na Julieth V. Rushuli. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti (Zanzibar) (Wagombea 3)- Sharim S. Khamis, Zainab B. Bakari na Ally Akalipo Ally. Nafasi za Ujumbe: Wawakilishi wa BAVICHA kwenye Mkutano Mkuu wa chama-nafasi 20 (Wagombea 39) na wawakilishi wa BAVICHA kwenye Baraza Kuu la chama-nafasi 5 (Wagombea 32). Wagombea waliorudisha fomu kwa nafasi za Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mratibu wa Uhamasishaji, Mweka Hazina watatangazwa katika ratiba ya baadaye.
MIKUTANO YA UCHAGUZI: Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wawakilishi wa BAVICHA kwenye baraza kuu na mkutano mkuu watachaguliwa na Mkutano Mkuu wa BAVICHA utakaofanyika tarehe 28 Mei 2011 kama ilivyotangazwa awali. Wagombea husika wanakumbushwa kufika kwenye mkutano mkuu kwa gharama zao. Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Mratibu wa Uhamasishaji na Mwekahazina watapendekezwa na Kamati ya Utendaji ya BAVICHA kwa mujibu wa ratiba itayopangwa baadaye na uteuzi wao utathibitishwa na Kamati Kuu ya chama hivyo wataalikwa katika vikao vya baadaye.
UCHUJAJI NA USIMAMIZI WA UCHAGUZI: Kwa mujibu wa katiba ya chama uchaguzi husika kwa kuwa ni wa kitaifa mkutano wake utasimamiwa na wazee wastaafu wa chama wakati katibu mkuu ndiye msimamizi wa uchaguzi katika taratibu zote kuanzia hatua ya awali. Aidha ngazi ya uchujaji itakuwa ni Kamati Kuu ya chama ambayo itafanya uteuzi wa wagombea katika kikao chake cha tarehe 26 Mei 2011 kwa kuwa ndiyo yenye wajibu wa kuyasimamia mabaraza kwa mujibu wa katiba na kanuni.
TARATIBU ZA KAMPENI: Kampeni za uchaguzi zitafanywa kwa kuzingatia kanuni za chama, maadili ya uongozi/viongozi (rejea kanuni za chama vifungu vya 10.1, 10.2 na 10.3) pamoja na muongozo juu ya uendeshaji wa uchaguzi ndani ya chama uliopitishwa na Baraza Kuu la Chama tarehe 13 Disemba 2007 unafafanua mambo yanayopaswa kufanywa na yasiyopaswa kufanywa wakati wa kampeni na uchaguzi ndani ya chama kwa lengo la kujenga mshikamano na umoja ndani ya chama na kufanya uchaguzi uwe huru na wa haki. Wagombea wote wanahimizwa kuzingatia taratibu za kampeni za uchaguzi ambazo nakala yake inapatikana pia kwenye mtandao wa chama www.chadema.or.tz kutokana na umuhimu wa uongozi wa vijana kwa mustakabali wa chama na taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya BAVICHA-Vijana; Nguvu ya Mabadiliko
John Mnyika (Mb)
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Vijana
0784222222