Chadema yasema vyama vyote vinafanya siasa vyuoni

Dodoma,

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (CHADEMA), amesema siasa vyuoni hazitakoma, endapo Serikali itashindwa kuwatimizia wanafunzi haki zao.

Alisema kila chama kinafanya siasa vyuoni na siyo kukitupia lawama Chama Cha Demokrasia na Maendeleo pekee, kwamba kinafanya siasa vyuoni.

Mbilinyi alitoa kauli hiyo bungeni jana, wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

“Sote tunaeneza siasa kwenye vyuo, mbona Nape (CCM), anazunguka kwenye vyuo na kufanya siasa na yeye siyo mbunge, hafadhari angekuwa mbunge basi.

Pia hapa bungeni Spika alitangaza kwamba kutakuwa na mahafali ya wanafunzi ambao ni wanachama wa CCM, Chuo Kikuu cha Dodoma akawa anawataka wabunge wa CCM waende kwenye mahafali hayo, hii yote ni kufanya siasa kama siyo siasa ni nini? alihoji Mbulinyi.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo aliitaka Serikali kuwalipa wazabuni wanapeleka vyakula kwenye shule za sekondari fedha zao wanazodai.

Alisema wazabuni wanaopeleka vyakula kwenye Shule ya Sekondari Iyunga wanadai fedha zao kwa muda mrefu lakini jambo la kushangaza ni kwamba Wizara imeendelea kukaa kimya.

“Kwanini hamuwalipi madeni yao, walipeni mbunge wao nifanye shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo kuchimba visima na siyo kutumia muda mwingi kufuatilia suala hili,” alisema Mbilinyi.

Mbunge wa Viti Maalum, Chiku Abwawo (CHADEMA), alisema Shule za Sekondari za Kata ni chanzo cha kuleta ukabira nchini.

“Shule hizi zinatupeleka kwenye ukabira hii inatokana na ukweli kwamba wanafunzi wanaosoma kwenye shule hizo ni wa eneo moja hivyo hawapati fursa ya kuchanganyikana na watu wengine,” alisema Abwao.

Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM), aliitaka Serikali kutoa mikopo ya elimu ya juu bure kwani hata inayotolewa sasa ni kazi bure kwani hakuna mpango madhubuti wa kuzirejesha.

“Wanafunzi wapewe fedha bure, kwani tunachofanya sasa ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu kwani fedha hizo hazirudishwi kwasababu vijana hawana kazi. Sasa kama hawana kazi hatalipaje, ni bora sasa wakapewa bure bila kusema kwamba wanakopeshwa,” alisema Chilolo.

Mbunge huyo pia aliitaka Serikali kuwalipa walimu madeni yao na kuongeza kwamba kuendelea kutowalipa ni aibu kwa serikali iwapo watatangaza mgogoro.

“Kwanini mnalimbikiza madeni haya, na kwanini mnamwamisha mwalimu kama hamna fedha za kumlipa hivyo fedha zitafutwe popote pale walimu hawa walipe fedha zao,” alisema.