CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimewatuhumu viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Jeshi la Polisi kwa kupanga njama ili kuwaunganisha viongozi wa juu wa Chadema kwenye kesi ya kumwagiwa tindikali, Mussa Tesha. Viongozi waliotajwa hadharani kuwa wanapanga mbinu hizo ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba na Ofisa wa Jeshi la Polisi makao makuu, Advocate Nyombi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Uenezi, John Mnyika alisema mikakati hiyo imesababisha kukamatwa kwa Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo wiki iliyopita na kupelekwa Igunga, mkoani Tabora kuunganishwa kwenye kesi hiyo.
Kileo alikamatwa na kupelekwa makao makuu ya Jeshi la Polisi ambako alihojiwa na jopo la maofisa wa polisi. Kwa mujibu wa Mnyika baada kuhojiwa aliwekwa mahali pasipojulikana na kwamba alizuiwa kuwekewa dhamana. Mnyika alisema siku iliyofuata, walielezwa kwamba Kileo alipelekwa Igunga kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka akituhumiwa kumwagia tindikali Tesha.
“Tumepata taarifa kwamba Kileo aliteswa vibaya na polisi ili awataje viongozi waliomtuma lakini alikuwa akibishana nao, lakini baadaye aliandikisha mambo waliyoyataka polisi,” alisema.
Akijibu tuhuma hizo, Nchemba alisema hakuna mikakati yoyote inayofanywa kati yake na Nyombi bali hiyo ni hofu yao viongozi wa Chadema kwa sababu wanafahamu kwamba walitenda kitendo hicho.
“Hatuhitaji kikao kudhihirisha hilo kwa sababu ni jambo lililo wazi kwamba Chadema walihusika katika kitendo hicho cha kumwagia tindikali mtu huyo,” alisema.
Kwa upande wake, Nyombi na Msemaji wa Polisi hawakupatikana kuzungumzia suala hilo, lakini Kamanda wa Mkoa wa Tabora, Peter Ouma alisema jeshi hilo litawasaka wahalifu popote walipo na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria bila kujali kama ni wanachama wa vyama fulani au la.
“Mhalifu anaweza pia kuwa mwanachama wa chama fulani kwa hiyo tukimkamata tusihusishwe na mambo ya siasa bali ni kufuata sheria,” alisema kuongeza kuwa Kileo bado hajafikishwa mkoani humo.”
Chadema imeunda jopo la mawakili saba wakiongozwa na Profesa Abdallah Safari na wengine ni Peter Kibatara na Gasper Mwalyela wanaoondoka leo kwenda Igunga wakati Mabere Marando, Tundu Lissu, Nyaronyo Kicheere na Method Kimomogoro watawafuata baadae.
CHANZO: www.mwananchi.co.tz