Siku chache baada ya Wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kususia hotuba ya ufunguzi wa Bunge iliyotolewa na Rais, Jakaya Kikwete, baadhi ya wabunge wapya wa chama hicho walioshiriki kitendo hicho, wameibuka na kusema hatua ile haikuwa utashi wao, bali kwa shinikizo la baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho.
Wabunge hao, wamesema iliwabidi kushiriki uamuzi ule kwa shingo upande, kwa kuhofia kuwa wasingeeleweka kwa viongozi wao na kuonekana wasaliti, lakini mioyoni mwao hawakuona mantiki yoyote ya kususia hotuba ya Rais ya ufunguzi wa Bunge, ikizingatiwa kuwa walikuwa mahali hapo kwa ajili ya kuwawakilisha wananchi waliowachagua.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutoandikwa majina yao gazetini kwa sababu zinazoeleweka, wabunge hao ambao hii ni mara ya kwanza kuingia bungeni baada ya kushinda wakati wa uchaguzi mkuu uliopita, walisema kitendo hicho ambacho kimepokewa kwa hisia tofauti na watu wengi, kimekidhalilisha chama chao badala ya kukisaidia.
Mmoja wa wabunge hao, alisema hapingani na chama chake kulalamikia matokeo yaliyompa ushindi Rais Kikwete, bali hakufurahishwa na uamuzi wa kuonyesha hisia hizo kwa kususia kikao muhimu cha ufunguzi wa bunge wakati Rais akihutubia.
Alisema kitendo hicho kimewachukiza wananchi wengi na kimejenga picha mbaya kwa wananchi kuwa chama hicho ni cha watu wenye visasi, wasio wavumilivu wa kisiasa na wanaopenda kutumia njia za mitafaruku kutatua matatizo badala ya njia za kidiplomasia.
Mbunge mwingine kijana wa chama hicho, alisema alitamani asishiriki kitendo cha kususia hutuba ya rais, lakini alishindwa kufanya hivyo, kwa kuwa baadhi ya viongozi wa juu walikuwa na msimamo mkali kuhusiana na suala hilo, hivyo asingeshiriki angejiweka katika mazingira magumu ndani ya chama.
“Unajua sisi bado ni wageni ndani ya chama na hili ndiyo bunge letu la kwanza, tusingeweza kwenda kinyume na matakwa ya viongozi wetu, japokuwa sisi wenyewe hatukufurahia jambo lile”, alisema mbunge huyo.
Mbunge mwingine mpya wa Chadema, ambaye hakutaka kuandikwa jina lake kwa kile alichosema kuepuka msuguano na viongozi wake, alisema kuwa kitendo hicho kimewafanya wabunge wa Chadema kueleweka vibaya kwa wapiga kura wao waliowatuma kwenda bungeni kuwawakilisha.
“Lazima tukubaliane na ukweli kuwa baadhi ya wananchi waliotuchagua kwenye nafasi ya ubunge kwenye urais waliamua kumpa kura Kikwete, sasa tunapomsusia tunakuwa hatueleweki tunaonekana kama tumewasaliti wananchi”.
“Hata ukiangalia wanaotuunga mkono kwenye jambo hili ni walewale walioonyesha kutuunga mkono tangu wakati wa kampeni, lakini kiukweli wananchi wengi hawajafurahia na hili si jambo jema. Lakini nadhani viongozi wetu watakuwa wamejifunza kitu, kwani binadamu tunajifunza kutokana na makosa”, aliongeza kusema mbunge huyo.
Aliongeza kusema kuwa, kitendo hicho kinaweza kuwapa wasiwasi wananchi kuwa wabunge wa chama hicho watatumia muda mwingi kuvutana na serikali badala ya kushughulikia matatizo yao na kutekeleza ahadi walizoahidi wakati wa kampeni.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi waandamizi na wabunge maarufu wa Chadema ambao inaelezwa hawakuunga mkono msimamo wa wenzao kususia hotuba ya Rais Kikwete hawakushiriki katika kitendo hicho.
Inaelezwa kuwa wakati wa kikao cha kujadili kama ipo haja ya wabunge wa chama hicho kususia hotuba ya rais au la kulitokea mvutano mkali, baadhi wakipinga na wengine wakiunga mkono msimamo huo.
Baadhi ya wabunge ambao hawakuingia kabisa bungeni siku lilipotokea tukio hilo kwa sababu ambazo hazijajulikana na hivyo kutoshiriki katika kitendo hicho cha kutoka nje ya ukumbi wa bunge ni, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zito Kabwe, Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, Mbunge wa Mpanda Said Arfi, Mbunge wa Viti Maalum Lucy Owenya.
Wabunge wa Chadema walisusa na kutoka bungeni wakati Rais Jakaya Kikwete anaanza kulihutubia Bunge kulifungua rasmi Alhamisi iliyopita.
Hali hiyo isiyo ya kawaida ilisababisha kelele bungeni zikiwemo za wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwazomea wenzao waliosusa.
Mara baada ya wabunge wa Chadema kutoka ukumbini, wabunge wa Chama Cha Wananchi (CUF) walikwenda kukaa kwenye viti vya waliosusa, Rais Kikwete akaendelea kuhutubia.
Katika hotuba yake, Rais Kikwete amesema, waliofanya hivyo wanapaswa kutambua kuwa hawana Rais, yeye ndiye Rais wao na kwamba hawana sehemu nyingine ya kupeleka mahitaji yao hivyo watakwenda, watarudi.
“Hata wale ambao hawakuichagua CCM bado hawana Rais, Serikali yao ni hii hii”, amesema Kikwete kabla ya kumaliza kulihutubia Bunge mjini Dodoma wiki hii.
Mara baada ya Rais kumaliza kulihutubia Bunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliwaeleza wabunge kuwa, baadhi ya vyama vimeanza kuonyesha mwelekeo usio sahihi.
Waziri Mkuu ametoa rai kwa Watanzania wasiruhusu mtu yeyote kuwagawa hivyo waseme hapana.
Kwa mujibu wa Chadema, wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu, kura za mgombea wao, Dk. Willbrod Slaa ziliibwa ili kumpa ushindi Kikwete.
Chama hicho kimesema, licha ya kutomtambua Kikwete, wabunge na madiwani wake wataendelea na kazi kama kawaida katika vyombo hivyo vya uwakilishi.
Wabunge wa Chadema pia wamekataa uteuzi alioufanya Kikwete kumteua Pinda kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania.
Kitendo hicho cha Chadema kimepokelewa kwa hisia mbalimbali na wananchi huku wengine wakisema kimetekeleza haki yao ya kidemokrasia, wengine wakilaani na kukieleza kuwa ni utovu wa nidhamu, kukosa busara na kutokamaa kidemokrasia.