CHADEMA Washinda Kata Zote Uchaguzi Mdogo Udiwani Arusha

Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Peter Slaa akizungumza.

Na Mwandishi Wetu, Arusha

HATIMAYE matokeo ya uchaguzi mdogo wa kata nne za Mkoani Arusha yamejulikana na taarifa ambazo mtandao huu umezipata, chama cha Chadema kimeshinda katika kata zote nne.

Kwa mujibu wa matokeo yaliorushwa na mtandao wa kijamii wa Kanda Ya Kaskazini unaomilikiwa na chama hicho, katika Kata ya Themi chadema imeshinda kwa jumla ya kura 678, huku CCM ikijipatia kura 326 na Chama cha CUF kikiambulia kura 313. Hivyo mgombea aliyeshinda katika kata hiyo ni Edmund Kinabo (Chadema).

Chadema pia imefanikiwa kutwaa Kata ya Kaloleni baada ya mgombea wake Kessy Emmanuel kushinda kwa jumla ya kura 1484, huku CCM ikijipatia kura 544 na Chama cha Wananchi, CUF kura 286. Kata nyingine ya Elerai pia imetwaliwa na Chadema baada ya mgombea wake Mhandisi James Mpinga kupata jumla ya kura 2047 na kuibwaga CCM iliyojipatia kura 1471.

Chama cha chadema kiliendeleza ushindi tena katika Kata ya Kimandolu baada ya mgombea wake udiwani kata hiyo, Mchungaji Rayson Ngowi kujipatia kura 2761 na CCM kuambulia kura 1166 huku CUF wakiambulia patupu katika kata hiyo kwa kura sifuri.

“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa amekuwa pamoja na sisi toka tunaanza (uchaguzi huo) mpaka tunamaliza, sasa tunajipanga kuijenga Arusha iwe kwenye hadhi ya GINEVA OF AFRICA, tunawashukuru wakazi wote wa Arusha na viunga vyake kwa kutuamini na kutuunga mkono na sasa ni MPERA MPERA MPAKA 2015 MJENGONI,” ilisema taarifa iliyorushwa katika mtandao wa CHADEMA KANDA YA KASKAZINI.