CHADEMA Wapigwa Marufuku Kutumia Helkopta Siku ya Uchaguzi

Helikopta inayotumiwa na Chadema kwa kampeni.

Helikopta inayotumiwa na Chadema kwa kampeni.


Na Bashir Nkoromo, Iringa

JESHI la Polisi, limekizuia chama chochote kutumia helkopta kwenye anga la Jimbo la Kalenga ikiea ni pamoja na kuwashughulikia kikamilifu kundi au yeyote atakayejaribu kusababisha au kufanya fujo wakati wa uchaguzi na utangazaji matokeo ya uchaguzi huo.

Onyo hilo limetolewa leo mjini Iringa na Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Ramadhani Mungi, wakati akieleza Polisi ilivyojiandaa kuhakikisha uchaguzi mdogo Jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, unafanyika kwa amani na utulivu, Jumapili hii, ya Marchi 16, 2014. Wakati onyo hili likitolewa Chadema ndiyo chama kinachotumia Helikopta na kilitamka kuitumia pia siku ya uchaguzi.

Kamanda Mungi alisema Jeshi la Polisi halitaki kuona Helikopta za vyama vyote zinazo ashiria kufanya kampeni siku ya kupiga kura ikiwa ni pamoja watu wasiokuwa na shughuli maalumu siku hiyo wakipitapita maeneo ya kupigia kura, kwani siku ya uchaguzi sio ya kufanya kampeni. Alisema wamepata taarifa kuwa baadhi ya viongozi wa vyama wameingiza maelfu ya watu mkoani Iringa kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha, Mbeya kwa visingizio vya kulinda kura zitakazo pigwa.

“…Sasa nataka niwaeleze kuwa sheria iko wazi kabisa, kila kituo cha kupigia kura kitakuwa na wakala wa chama kinachoshiriki katika uchaguzi huo na hao ndio wawakilishi wa chama hicho na walinzi halali wa uchaguzi ni askari wa Jeshi la Polisi. Kufuatia hali hiyo mambo yafuatayo yanasisistizwa sana,” alisema.

“…Sisi Polisi Mkoa wa Iringa tunataka wananchi wa Kalenga wapinge kura kwa  amani na utulivu mkubwa siku ya Jumapili tarehe 16/3/2014. Hii ndio dila  yetu na tutahakikisha tunafika hapo.”

Akizungumzia taarifa mbalimbali za malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo alisema mengine yamekuwa ya kiuhasama na ushindani hivyo wamekuwa wakiyachambua kadri inavyohitajika kabla ya kuyafanyia kazi.

“…Tarehe 4/03/2014 nilifuatwa tena na baadhi ya waandishi na kunieleza kuwa siku hiyo waliitwa na CCM na kuelezwa kuwa siku ya tarehe 27/2/2014 walitegewa misumari katika kijiji cha WASA ili mabasi yaliyokuwa yamebeba wafuasi wao yaweze kutobolewa magurudumu yake, pia nao walisema tukio hilo halijaripotiwa Polisi. Mimi nilikataa kulizungumzia swala hilo.

“…Vitendo vilivyofanywa na vyama hivyo vililenga kuanzisha propaganda za kisiasa kwa kutumia uhalifu kwa kupitia vyombo vya habari. Sisi Polisi tulibaini hali hiyo na ndiyo sababu tuliamua kuwa kimya na nyinyi wenzetu kwa kuzingatia maadili ya kazi zenu pia mlikaa kimya. Kuanzia hapo vyama vilianzisha mashindano ya kuripoti kesi zao Polisi. Leo hii vyama hivyo vimeripoti kesi ishirini na moja ambazo zilisababisha kukamatwa kwa wafuasi (19) wa vyama hivyo viwili.”

“…Ndugu waandishi, kati ya kesi hizo ishirini na moja, kesi kumi na tisa (19) zile ambazo hazina madhara ya moja kwa moja kwa binadamu ama mali, kesi hizo ni  zile ndogondogo sana, kama vile kuchana mabango, kuteremsha bendera, kuchana vipeperushi, kutukanana n.k. kesi tatu zilikuwa zile zenye madhara kwa binadamu na mali ambazo ni kupigana hadharani, kujeruhi na kuharibu mali. Kati ya kesi ishirini na moja (21), kesi kumi upelelezi wake umekamilika na majalada yake yamefikishwa kwa mwanasheria wa serikali.”

Alisema katika kesi walizopokea Jeshi la Polisi limebaini mambo mengi hivyo yaliyohitaji kufanyiwa kazi ilifanyika hivyo; “Mfano CHADEMA kilikuwa kikitoa malamiko kuwa tumeacha kumkamata ndugu Hassan Mtenga mtuhumiwa wa kesi moja iliyokuwa imefunguliwa dhidi yake.”

“Shutuma hizo hazina msingi kwani kesi iliyofunguliwa dhidi ya mtu huyo haikuwa ya jinai bali ya madai na tuliwajulisha hivyo. Nia ya kufanya hivyo ilikuwa kuifanya jamii iamini kuwa Polisi ni dhaifu na wenye kuonesha upendeleo katika kushughulikia kesi za uchaguzi. Nashukuru Polisi tulikuwa watulivu, hatukujibu na jamii imetuelewa sana.”

“…Ndugu waandishi, pamoja na matukio hayo polisi tumekuwa tukipokea taarifa za vitisho vya kuwepo kwa watu mbalimbali kutoka kwa vyama vyote walioingizwa mkoani humu kwa nia ya kutenda vitendo vya uvunjifu wa amani. Hatutaki kuona walinzi wa chama  chochote  katika Jimbo la Kalenga. Jukumu la kulinda uchaguzi, maisha na mali ya wana Kalenga ni la Jeshi la Polisi,” alisema Kamanda Mungi.