*Lema amfananisha na ‘mlevi’, asema anaendesha propaganda chafu
Na Mwandishi Wetu, Arusha
CHAMA cha CHADEMA pamoja na Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini wa chama hicho, Godbless Lema wamemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tedwa kuacha kutumiwa na CCM kwa kufanya propaganda chafu.
“Nina mashaka wataki Tendwa anaongea na waandishi wa habari juzi alikuwa amelewa pombe maana siyo akili yake, naye ameanza kusaidia CCM kufanya propaganda chafu labda ni vema akatambua wajibu wake na sio kuanza kufanya kazi za siasa za CCM,” alidai Lema kupitia taarifa
aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana
Lema alisema kuwa yeye kama Mbunge ana wajibu wa kutoa matumaini
kupitia chama chake kwa Watanzania wote na na hatasita “kutinga”
Jimbo hilo la uchaguzi kufanya kampeni, ambazo zinadaiwa kumkataza
kushiriki kwa propoganda za kukatwa shingo (kuuwawa)
“Pia Namwambia Tendwa ni vema akajua kuwa yoyote anayeitetea uovu leo itakuwa hasara kwake, au kwa familia yake kesho, ni wito wangu kwa kila kijana wa Arumeru anayeishi maeneo ya mjini kuona fursa hii ni kwa ajili ya ukombozi wan chi yetu na siyo kwa Arumeru pekee hivyo kwenda vijijini kwenda kutoa elimu tulikoacha wazee wetu”
“Tunawatia moyo wale mlioko mbali lakini wapenda mabadiliko, sisi
tulioko huku tutapambana kwa niaba yenu kufa na kupona kuhakikisha
haki, usawa na demokrasia vinapata thamani halisi, hakika hatutakubali
nguvu ya udhalimu wlaa rushwa iwachagulie ndugu zetu wa arumeru
Mbunge, kama mbunge wa CCM Mwigulu Nchemba, alivyotamba katika hoteli ya Mt. Meru kuwa pesa bado hazijaanza kumwagwa kwani ndiyo kwanza ziko njiani zinakuja,” alisisitiza Lema.
Naye Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, akizungumza kwa njia ya simu, alisema kuwa amesikitishwa na kauli za Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kwa kuzingatia propaganda za mitandao ya kijamii na kukurupuka kwa kueleza waandishi wa habari badala ya kuzifanyia kazi. Katibu huyo alisema kuwa vurugu anazodai Msajili kuwa zilifanywa na Lema siyo kweli bali zilianzishwa na vijana wa CCM baada ya kumuona Lema akipita wakalipuka kwa shangwe na hamaki ikatokea kwa vijana hao.
Alidai kuwa baada ya tukio hilo lililotokea msibani, walikutana na
viongozi wa CCM wakazungumza na kuweka sawa, ila wanapoona leo
yanakuja kwa sura ya wazee wa kimila Washiri wameshangazwa na maneno hayo aliyoyatoa.
“Mimi kama katibu wa Chama jana nilikutana na wazee toka katika kata
tano, na nikazungumza nao ambapo kikubwa wanachodai ni siasa za
ukombozi wa jimbo hilo ambalo limeangamizwa na CCM kwa kipindi cha
miaka 15 kwa kuwajaza masetla wanaomiliki ardhi na maji huku wananchi wakibaki wanahangaika,” alisema Golugwa
Alidai kuwa Lema hakuwahi kusema neno baya lolote kama inavyodaiwa na propaganda za Tendwa na CCM, ila wao kama Chama watashirikiana na Washiri na wakazi wote wa Meru bali Propoganda hawatazipa nafasi katika kampeni hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alipoulizwa
ofisini kwake kuhusiana na vitisho vya kukatana mapanga kwenye
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru, alisema kuwa jeshi
limejiandaa kuhakikisha amani inakuwepo katika jimbo hilo.
Andengenye alisema kuwa mapanga hutumika kwa ajili ya kukatia migomba na majani na si kwa ajili ya kupigana na kuongeza kuwa polisi
wamejiandaa vizuri kuhakikisha kunakuwa na amani na kila mwananchi
kutumia haki yake kidemokrasia kuingia na kutoka Meru bila kudhurika.