CHADEMA wafunika Igunga, Dk. Slaa ‘amnanga’ Mkapa

Katibu Mkuu CHADEMA, Dk Willibroad Slaa

Na Mwandishi Wetu, Igunga

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kilifunga mitaa kadhaa kwa kuwa na umati wa wanachama, wapenzi na wafuasi wa chama hicho mjini hapa wakati wa maandamano kuzindua kampeni zake za kuwania ubunge Jimbo la Igunga.

Waandamanaji hao wakiongozwa na viongozi wa kuu wa Chama hicho, Freeman Mbowe, Dk. Wilbroad Slaa na viongozi wengine pamoja na wabunge wake, walipokelewa katika Kijiji cha Hanihani na maandamano kuendelea hadi Uwanja wa Sokoine mjini Igunga.

Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, alianza kwa kumshambulia Rais mstaafu Benjamin Mkapa kuwa hana sifa za kuzindua kampeni za CCM kutokana na kuwa na tuhuma nyingi. Alimtuhumu Mkapa kuwa alidiriki kufanya biashara akiwa Ikulu huku akishiriki katika baadhi ya tuhuma za ufisadi hali ambayo imechangia Watanzania kuendelea kuwa masikini.

Aidha Dk. Slaa alimtuhumu Mkapa kuhusika pia kuiweka nchi gizani kwa kukosa umeme hadi sasa, jambo ambalo aliwashauri wana-Igunga wamuulize maswali juu ya hali zote ngumu za maisha kwa sasa, kwani yeye amechangia hali hiyo. “…Mkapa amefanya biashara akiwa Ikulu kupitia kampuni ya ANBEM aliyoianzisha na kufanikiwa kuununua mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira…,” alimtuhumu Dk. Slaa na kuongeza kwamba; “Mkapa hana jeuri ya kuzindua kampeni hapa Igunga, nilishamsema sana bungeni.”

Alisema Serikali iliyopo madarakani (CCM) haija jipya zaidi ya kuwalaghai Wananchi kila mara, alitolea mfano hivi sasa bei ya Sukari imepanda kupindukia maeneo mbalimbali lakini imeshindwa kudhibiti hali hiyo.
Alisema anashangaa kuona CCM inajiandaa kusherehekea miaka 50 ya uhuru, ilhali wananchi hawana cha maana cha kujivunia.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CHADEMA Igunga, Joseph Kashindye aliitaka CCM kutambua kuwa si watumishi wote wa Serikali wanakubaliana na madudu yanayofanywa serikalini bali wapo wanaoguswa na kuchukizwa na hali hiyo.

Kashindye alisema chama alichojiunga nacho ni makini na kinaweza kuleta mabadiliko, na kudai CCM kwa sasa inakufa hivyo si chama cha kujiunga nacho. “CCM ni chama kinachokufa ndio maana sijajiunga nacho…,lakini ukiona mwalimu ameacha chaki na kuingia kwenye siasa ujue hali ni mbaya, mambo ni hovyo, Mwalimu Nyerere aliacha ualimu na kuingia kwenye siasa na mimi nimeamua kufuta mfano wa Mwalimu Julius Nyerere,
nataka nikaingie bungeni kusimamia masilahi ya wana-Igunga,” alisema.

Naye Mbowe alisema anashangaa kuona hali ya umasikini kwa Watanzania inaendelea kuwa mbaya kadri miaka inavyo kwenda, huku Serikali iking’ang’ania madarakani. Alisema Tanzania si nchi ya kuzunguka ikiomba misaada kama anavyofanya Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi.

Alisema Tanzania ina rasilimali nyingi hivyo endapo viongozi watazitumia vizuri, haliwezi kuwa taifa la kuombaomba hovyo. “Rais anazunguka nje ya nchi akiomba vyandarua vya mbu, huku wawekezaji wanaondoka na rasilimali za nchi…,” alisema Mbowe.