Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kuwa kinaandika barua ya malalamiko kwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Arumeru Mashariki, Trasias Kagenzi, dhidi ya Meneja kampeni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Nchemba, kwamba amekutwa katika ofisi ya serikali ya kijiji cha Maji ya Chai akiendesha vikao vya chama na mabalozi wa nyumba kumi.
Meneja kampeni wa Chadema katika kampeni za uchaguzi mdogo wa ugunge Jimbo la Arumeru Mashariki utakaofanyika Aprili Mosi, Vincent Nyerere, alisema kuwa, Chadema kimesikitishwa kuona ofisi ya serikali ambayo kimsingi ndiyo inapaswa kusimamia uratibu wa uchaguzi kwa ngazi ya kata, inatumiwa kuendesha vikao vya CCM.
“Hapa ni wazi hawa wenzetu (CCM) wameanza kucheza rafu kama za Igunga na sisi hatuzihitaji rafu hizi na tunaandika barua ya malalamiko kwa msimamizi wa jimbo la uchaguzi, kwa sababu hiyo tumekosa imani na mtendaji wa kijiji hiki cha Maji ya Chai,” alisema Nyerere.
Alisema kuwa wao walikuwa wakitoka katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru kumsindikiza mgombea wao, Joshua Nassari, kwa ajili ya kuhakikiwa kwa fomu yake na kutoa uthibitisho wa aliyoandika katika fomu ya kugombea ubunge kabla ya kurudishwa kwa msimamizi wa uchaguzi leo na ndipo walipomkuta Nchembe akiwa katika vikao na makada hao wa CCM katika ofisi ya serikali.
“Hizi ni vurugu hivyo kama CCM wanataka amani, tafadhali wasianze rafu za Igunga kuzileta Arumeru, kwa kweli hatutakubali, tutakula sahani moja na hili tuna ushahidi na tuko tayari kulitolea ushahidi,” alisema Nyerere, ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini.
Aidha, Nyerere alisema kuwa Chadema wanatarajia kuzindua kampeni zao rasmi Jumamosi asubuhi asubuhi ambazo zitazinduliwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Alisema kuwa uzinduzi huo utakwenda sambamba na maandamano yatakayotokea Arusha mengine yatatoka KIA na yote yatakutana eneo la Usa River katika viwanja vya eneo la mkutano.
“Mkutano huo utazinduliwa kwa kishindo kwa helkopta, magari, baiskeli na pikipiki, vyote vikiwa vinapeperusha bendera za Chadema, hivyo nawaomba wapenzi wa Chadema wafike eneo husika mapema kushuhudia uzinduzi huo,” alisema Nyerere.
Nyerere alisema kuwa Chama chao kitafuata taratibu zote za sheria ya maandamano kwa kuelekeza wafuasi wao kutii amri ya barabarani kwa kutembea upande mmoja wa barabara na kuyaachia magari kupita na kumaliza mikutano yao kwa wakati uliopangwa wa kumalizika kwa kampeni za uchaguzi.
Kwa upande wake Katibu wa CCM wa Wilaya ya Arumeru, Edson Lihwehuli, alipoigiwa simu ili kuzungumzia madai hayo, alitata simu. Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi, hakupatikana kujibu madai hayo.
Hata hivyo, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mery Chatanda, alisema kwa kuwa Nchemba ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, anazifahamu taratibu za chama. Alisema kuwa ana haki ya kufanya vikao vya ndani na mabalozi kwa kuwa kampeni hazijaanza. Hata hivyo, alisema kuwa hana taarifa kama Nchemba alikutana na mabalozi hao katika ofisi ya serikali.
Kwa upande wake, msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi, alisema hadi jana jioni alikuwa hajapokea barua ya malalamiko kutoka Chadema.
CHANZO: NIPASHE