Na Mwandishi Wetu
KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni aliyekuwa akitakiwa kukamatwa kwa amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya mjini Arusha amekamatwa jijini Dar es Salaam.
Taarifa zilizoufikia mtandao huu zilieleza Mbowe tayari anashikiliwa na polisi wa jijini Dar es Salaam, kutekeleza amri ya mahakama ya Arusha ambapo Mbowe anakabiliwa na kesi pamoja na viongozi wengine wa chama cha CHADEMA.
Wakati taarifa za kukamata kwa Mbowe zikitoka, taarifa nyingine kutoka mkoani Singida zinaeleza Jeshi la Polisi mkoani humo zinamshikilia mbunge Kabwe Zitto kwa tuhuma za kufanya mkutano eneo hilo na kupitiliza saa za kawaida kisheria.
Hata hivyo taarifa kutoka kwa Zitto mwenyewe alisema anashangazwa na hatua ya polisi kumkamata tena akidai akiwa hotelini alipofikia baada ya mkutano wake, jambo ambalo alilitilia mashaka.
“Polisi walitoa amri nifunge mkutano na nikafunga mkutano. Wamenifuata hotelini kunikamata na nipo kituoni. Nimekataa kutoa maelezo yeyote mpaka awepo mwanasheria wangu na kuthibitisha kama wamefuata taratibu kumkamata Mbunge..,” aliuandikia mtandao huu mbunge huyo.
Taarifa zaidi zilieleza baada ya mbunge huyo kukataa kutoa maelezo yake alikuwa aendelee kushikiliwa na polisi, lakini hadi taarifa hii inachapishwa haikuweza kujulikana kama anaendelea kushikiliwa au la.
Juhudi za kumpata Mbowe kuzungumzia taarifa za yeye kushikiliwa na polisi hazikuweza kupatikana mara moja, japokuwa ilikuwa ikijulikana wazi kuwa alikuwa akitafutwa na polisi kutekeleza amri ya
mahakama iliyotolewa hivi karibuni mjini Arusha