Na Mwandishi wa Thehabari, Dodoma
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tindu Lissu (CHADEMA), amesema Serikali isipomfikisha Mahakamani aliyekuwa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Andrew Chenge CHADEMA watakwenda mitaani kushtaki kwa wananchi.
Amesema kwa mujibu wa sheria za sasa cha Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Chenge anaweza kushtakiwa kwa kuwa ndiye mtuhumiwa namba moja wa kashfa ya Rada.
Lissu alitoa kauli hiyo mjini hapa juzi baada ya Serikali kumsafisha na kueleza kuwa Chenge na Dk. Idris Rashid wametajwa kuhusika katika rushwa ya rada ya sh. Bilioni 40 hivyo lazima washitakiwe.
Alisema serikali inajua kuwa Chenge alihusika, na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliambiwa ukweli wote kwa barua ya Taasisi ya Uchunguzi wa Makosa Makubwa ya Jinai (SFO) ya Uingereza, lakini serikali kupitia Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mathias Chikawe, ameamua kuwadanganya wananchi kwa kusema kuwa hakuna ushahidi wa kumshitaki Chenge.
“Ushahidi upo hivyo Chenge na Dk. Rashid lazima washtakiwe kwa upotevu wa fedha za Watanzania kinyume na hapo sisi tutakwenda kwa wananchi kushtaki,” alisema Lissu.
Juzi Kamati ya Bunge ya iliyokuwa imeenda Uingereza kufuatilia fedha za Rada ilimkabidhi, Spika Anne Makinda ripoti na kutoa mapendekezo ya waliohusika kwenye sakata hilo washtakiwe.
Pia iliitaka Serikali kuishtaki Kampuni ya BAE system ya Uingereza iwapo itashindwa kuilipa Tanzania paundi milioni 29.5 kabla ya Septemba mwaka huu kama ilivyoamriwa na mahakama.
Wakati maoni ya Kamati ya Bunge yakiwa hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Mathias Chikawe, alimsafisha Chenge, ambaye amekuwa akituhumiwa kuhusika kwenye kashfa hiyo.
Chikawe alieleza kuwa Chenge hana hatia na kamwe Serikali haiwezi kumpeleka mahakamani kwa kuwa yanayozungumzwa juu yake ni hisia.
Chikawe aliliambia Bunge juzi jioni kuwa SFO ilipochunguza kashfa hizo haikuonesha uhusika wowote wa Chenge kwenye sakata hilo .
“ Kama yupo mtu yeyote anayeona SFO au Takukuru haikufanya kazi yake vizuri, atuletee ushahidi sisi tutamshtaki Chenge hata kesho, hatuwezi kwenda mahakamani kwa hisia ndio maana hatujamshtaki Chenge,” alisema Chikawe.
CHANZO; Jambo Leo.