Na Janeth Mushi, Arusha
IKIWA ni siku chache tangu uongozi wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA), Arusha Mjini mkoani hapa kujiuzulu, uongozi wa chama hicho mkoani hapa umeiomba Kamati Kuu ya chama hicho kuwafukuza madiwani wake sita katika Wilaya ya Arusha Mjini.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo mjini hapa Mwenyekiti wa
CHADEMA mkoani hapa, Samson Mwigamba amesema madiwani hao
wamekaidi agizo la Kamati Kuu lililowataka kujiuzulu nafasi zao
kufuatia muafaka wa U-meya katika Jiji la Arusha, kwa kile kufikia muafaka kinyume na taratibu za Chama hicho.
Alisema wajumbe wa mkutano huo wamesikitishwa na kitendo cha madiwani hao kukaidi agizo la Kamati Kuu lililowataka kujiuzulu nyadhifa zao kufuatia muafaka batili wa Umeya jijini hapa na kuomba radhi kuwa kuingia na kukubali muafaka huo bila kushirikisha chama na kuwa kinyume na taratibu za chama.
“Wajumbe wa Mkutano Mkuu wamekubaliana madiwani hao wafukuzwe kwa maana hawana nidhamu kwa chama na wanahatarisha umoja na usalama ndani ya chama, kwani muda wa kuomba msamaha umeshapita walipewa nafasi ya kwanza ila hawakuitumia vizuri, walipewa mwongozo ambao uliwapa siku 3 na kushindwa kuomba radhi kwa muda huo,” alisema Mwenyekiti huyo.
Aliwataja madiwani hao kuwa ni Estomih Mallah ambaye ni Naibu Meya wa Jiji la Arusha, John Bayo Diwani wa Kata ya Elerai, Reuben Ngowi diwnai wa Themi, Crispin Tarimo (Sekei), Charles Mpanda(Kaloleni) na Rehema Mohamed diwani wa viti maalum.
Mwigamba alisema kuwa hatua ya kamati ya uongozi wa ngazi ya wilaya kujiuzulu ni sahihi kwani kamati hiyo ilishindwa kutimiza wajibu wake na kudai kuwa huo ndio chanzo cha mgogoro uliopo hivi sasa.
Alisema kuwa Chama hichongazi ya wilaya kiliitisha mkutano kujadili hali ya kisiasa ya wilaya hiyo hususani muafaka wa madiwani wa CCM na CHADEMA katika manispaa ya Arusha na kujiuzulu kwa wajumbe wa kamati ya utendaji wa chama hicho.