CCM Yawaadhibu Lowassa, Sumaye, Membe na Wassira…!

Walioadhibiwa ni waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye,  mawaziri Benard Membe, Stephen Wassira na Naibu Waziri, January Makamba pamoja na aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja.

Walioadhibiwa ni waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, mawaziri Benard Membe, Stephen Wassira na Naibu Waziri, January Makamba pamoja na aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja.

Na Joachim Mushi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) hatimaye kimeanza kuchukua hatua kwa wanachama wake 6 nguli walioonekana kuanza kampeni za kugombea urais ndani ya chama hicho mapema kabla ya muda kutangazwa. Walioadhibiwa ni pamoja na waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, mawaziri Benard Membe, Stephen Wassira na Naibu Waziri, January Makamba pamoja na aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari toka CCM na kusainiwa na Katibu Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi NEC Taifa, Nape Nnauye alisema makada wote 6 wa CCM waliohojiwa wamekutwa na makosa hivyo kupewa adhabu ya onyo na chama. Alisema makada hao 6 wa CCM pia watakuwa chini ya uchunguzi wa mwaka mmoja wakiangaliwa mwenendo wao ili kujirekebisha.

Vigogo hao wa CCM, Edward Lowasa, Frederick Sumaye, Bernard Membe, Stephen Wassira, January Makamba na William Ngeleja walihojiwa na sekretarieti ya CCM mjini Dodoma kabla ya kubainika na makosa, kabla ya Tume ya Udhibiti na Nidhamu kuwajadili na hatimaye Kamati Kuu ya CCM ambayo ilitoa adhabu hiyo kwa wahusika.

Nape alisema baada ya kuhojiwa wote walithibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea Urais kabla ya wakati jambo ambalo ni kinyume na Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).

“…Wamethibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya Chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii. Kosa hili nalo ni kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara kadhaa za kanuni hizo,” alisema Nnauye.

“Kamati Kuu baada ya kuthibitisha makosa hayo imewapa watu wote sita waliohojiwa adhabu ya onyo kali na kuwataka wajiepushe na vitendo vinavyokiuka maadili na iwapo wataendelea na vitendo hivyo Chama kitawachukulia hatua kali zaidi. Tafsiri ya adhabu ya ONYO KALI kwa mujibu wa Kanuni za Uongozi na Maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara ya 8(ii) (b) ni; “Mwanachama aliyepewa adhabu ya ONYO KALI atakuwa katika hali ya kuchunguzwa kwa muda usiopungua miezi 12, ili kumsaidia katika jitihada zake za kujirekebisha.” Ilieleza taarifa ya Nnauye.

Aidha alifafanua kuwa Kamati Kuu imeitaka Kamati Ndogo ya Udhibiti kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kuwa mawakala na wapambe walioshirikiana na makada hao walioadhibiwa nao kuchukuliwa hatua.

“…Kamati Kuu imewaonya vikali Viongozi na Watendaji wa Chama na kuwataka kujiepusha kujihusisha na matendo ya wanawania Urais yanayovunja na kukiuka maadili ya Chama, wametakiwa kuzingatia Kanuni na taratibu za Chama.”