HALMASHAURI Kuu ya CCM Taifa katika kikao chake cha siku moja chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Taifa Dr. Jakaya M. Kikwete, pamoja na mambo mengine imetoa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa CCM kwa uchaguzi mdogo wa jimbo la Arumeru Mashariki.
Katika kikao chake hicho kilichofanyika tarehe 12/02/2012 mjini
Dodoma, NEC pia imetoa ratiba ya mchakato wa kuwapata wagombea udiwani kwa tiketi ya CCM kwenye kata nane zilizotangazwa kufanya chaguzi Ndogo na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
1. UBUNGE:
Katika nafasi ya Ubunge kwa Arumeru Mashariki, utaratibu utakaotumika
ni ule wa kupiga kura za maoni kwenye Mkutano Mkuu wa Jimbo.
(i) Tarehe 13 – 18/02/2012 Kuchukua na kurejesha fomu.
(ii) Tarehe 20/02/2012 Mkutano Mkuu wa Jimbo kupiga Kura za maoni.
(iii) Tarehe 21/02/2012 Kamati ya Siasa ya Wilaya kujadili Wagombea na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa.
(iv) Tarehe 24/02/2012 Kamati ya Siasa ya Mkoa kujadili Kutoa
mapendekezo yake kwa Kamati kuu.
(v) Tarehe 27/02/2012 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kufanya
uteuzi wa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi.
2. UDIWANI
Nafasi ya Udiwani katika kata 8 za Tanzania Bara Katika nafasi hii
kura za maoni zitapigwa kwenye Mikutano Mikuu ya Matawi.
(i) Tarehe 13 – 16/02/2012Kuchukua na kurejesha fomu.
(ii) Tarehe 17 – 21/02/2012 Kampeni za Uchaguzi kwenye Matawi.
(iii) Tarehe 22/02/2012Mikutano Mikuu ya Matawi kupiga kura za maoni.
(iv) Tarehe 25/02/2012 Kamati za Siasa za Wilaya kujadili wagombea na
kutoa mapendekezo yake kwa Kamati za Siasa za Mikoa.
(v) Tarehe 27/02/2012 Kamati za Siasa za Mikoa kujadili wagombea na
kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu za Mikoa.
(vi) Tarehe 29/02/2012 Halmashauri Kuu za Mikoa kufanya uteuzi wa wagombea.
Katika hatua nyingine Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imepokea maelezo
juu ya mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya na maelezo juu ya mgomo
wa madaktari nchini.
Kwa ujumla NEC imepokea maelezo hayo kutoka serikalini na kuiagiza
serikali kukamilisha mchakato wa kumaliza kabisa mgogoro wa madaktari
nchini na kuhakikisha migogoro ya namna hiyo inashughulikiwa mapema
ili isiwe na madhara makubwa kwa wananchi.
NEC imeridhishwa na jinsi mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya
unavyoendelea na kuipongeza serikali kwa jinsi inavyolisimamia swala
hilo. Imewataka wana CCM na wananchi wote kushiriki mchakato huo, huku wakizingatia kutunza amani na utulivu uliopo nchini.
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imewapongeza viongozi, wanachama na
wananchi wa Mkoa wa Mwanza kwa jinsi walivyofanikisha sherehe za miaka 35 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi ambapo kitaifa mwaka huu zilifanyika mkoani humo.
Sherehe hizo ziliandaliwa na kufanikiwa kwa kiwango cha hali ya juu
kabisa, hivyo NEC inawapongeza kwa kufanikisha sherehe hizo.
Pamoja na Mkoa wa Mwanza NEC inawapongeza wanachama, viongozi na wananchi kwa ujumla nchi nzima kwa jinsi walivyofanikisha sherehe hizo za miaka 35 ya kuzaliwa kwa CCM kwenye maeneo yao.
Imetolewa na;
Nape Moses Nnauye
Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa
Itikadi na Uenezi