CCM Yatangaza Siku ya Kumkabidhi Uenyekiti Rais Magufuli

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM.

Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete (katikati) akiwa na baadhi ya viongozi wa juu wa CCM.

Na Joachim Mushi, Dar es Salaam

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) leo kimetangaza tarehe ya kumkabidhi rasmi uongozi wa chama, Rais John Pombe Magufuli ikiwa ni utaratibu wa kawaida ndani ya chama hicho. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi leo jijini Dar es Salaam kwa wanahabari, Christopher Ole Sendeka Mkutano Mkuu Maalum wa CCM utafanyika Julai 23, 2016.

Alisema uamuzi wa kufanyika kwa mkutano huo umefikiwa baada ya Kikao cha Kamati Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete kilichofanyika Ofisi Ndogo ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam. Alisema Mkutano huo Mkuu Maalum utatanguliwa na vikao vya sekretarieti, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa.

“…Lengo la Mkutano Mkuu huo Maalum ni kukabidhiana kijiti cha uongozi wa juu wa chama chetu kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM Dk. Kikwete ambaye pia ni Rais mstaafu wa Awamu ya Nne kwenda kwa Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli kama ulivyo utamaduni wa CCM,” alisema Ole Sendeka.