CCM yaridhia kuondoka madarakani kwa Rostam, yataka wengine wafuate nyayo


Katibu Mkuu wa CCM Taifa Willson Mkama,akisoma utaratibu wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya CCM Taifa kilichofanyika hivi karibuni Dodoma,(wa pili kulia) Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete, makamo wa Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Amaan Abeid Karume, Rais wa Zanzibar na Mjumbe wa Kamatiu Kuu ya CCM Dk. Ali Mohamed Shein, wakisikiliza kwa makini taarifa hizo.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeridhishwa na hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Rostam Aziz na kuwataka walengwa wengine waliotakiwa kujipima na kujiuzulu kufanya hivyo mara moja.

Msimamo huo umetolewa Agosti Mosi katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kilichomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, ambacho kiliongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho.

Hata hivyo kitendo cha CCM kuridhia na kupongeza kitendo cha kujiuzulu kwa Rostam, kinaleta utata mpya ndani ya chama hicho, kwani licha ya Rostam kujiuzulu hakuridhishwa na zoezi linalofanywa na timu ya Sekretarieti ya CCM dhidi ya dhana nzima ya kujivua gamba, ambayo inaongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi, Nape Mnauye.

Rostam katika hotuba yake ya kujiuzulu amekilaani kitendo cha dhana hiyo kinachowalenga wao, badala ya chama kizima hivyo kuamua kujiondoa jambo ambalo linaonesha wazi hajapendezwa na kazi ya akina Nape.

Hata hivyo katika taarifa iliyotolewa na CCM baada ya kikao cha Kamati Kuu kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Nape. Inapingana na mtazamo wa Rostam kwani Kamati Kuu imepongeza kazi inayofanywa na Sekretarieti yake ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM chini ya akina Nape; kwamba wanafanya kazi nzuri na waongeze bidii.

“Kamati Kuu imepokea na kuridhia taarifa ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Ndugu Rostam Aziz. Aidha imempongeza kwa uamuzi huo uliozingatia maslahi mapana ya chama chake. Kamati Kuu inaagiza chama kupanga ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea ubunge wa Jimbo la Igunga itakayozingatia ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi juu ya uteuzi wa mgombea,” imesema taarifa ya CCM.

Aidha Kamati Kuu imefanya uteuzi wa makatibu 27, kujaza nafasi zilizokuwa wazi katika wilaya hizo. Pamoja na uteuzi huo, Kamati Kuu imetengua uteuzi wa Makatibu wa Wilaya watatu (3) katika kuboresha ufanisi wa kazi katika wilaya hizo.

Aidha Kamati Kuu imejadili masuala mengine kama; migogoro ya ardhi, tatizo la bei ya pamba, tatizo la uuzaji wa mahindi, migogoro migodini, masuala yanayohusu kero za Muungano na kuagiza Serikali kuyashughulikia kwani yanatatulika.

Pamoja na hayo Kamati Kuu, imejadili na kupitisha miundo mipya ya Idara ya Itikadi na Uenezi na Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa. Kuhusu suala la maadili ndani ya Chama, Chama kinaendelea kusimamia maadili, na kuwataka wale waliotakiwa kujipima na kuwajibika watumie muda huo, kujipima na kuwajibika kwa masilahi mapana ya chama.

Hata hivyo Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inatarajiwa kukutana wakati wowote mwezi Septemba, ambapo pamoja na mambo mengine itatathimini utekelezaji wa maamuzi yake.