Na Mwandishi Wetu
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimempitisha rasmi mtoto wa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete kugombea Jimbo la Chalinze kwa tiketi ya chama hicho. Ridhiwan Kikwete aliyeshinda kura ya maoni iliyofanyika katika jimbo hilo hivi karibuni sasa atapeperusha bendera ya CCM kugombea jimbo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na kusainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye, Ridhiwan amepitishwa rasmi na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa iliyokutana mjini Dodoma kujadili masuala kadhaa ya chama hicho.
Uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Chalinze kuziba nafasi iliyoachwa wazi na mbunge wa zamani wa jimbo hilo, marehemu Said Mwanamdogo, unatarajiwa kufanyika Aprili 6, 2014. Taarifa ya CCM imeeleza kampeni za chama hicho zitazinduliwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahaman Kinana na kufungwa na Makamu wa Rais, Dk Gharib Bilal.