CCM yalia msiba wa Chadema, yakanusha kuhusika

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa mawakala wa CHADEMA, Mbwana Masoud kilichotokea baada ya upigaji kura katika uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Igunga mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano na Umma, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM kwa vyombo vya habari inasema; kifo hicho kinasikitisha, na hasa ukizingatia mazingira yake kutatanisha na kuacha maswali mengi kwa umma. Hadi sasa haijajulikana chanzo cha uhakika juu ya kifo cha kijana huyo.

“CCM inaungana na Watanzania kuomboleza msiba huo, na kutoa pole kwa familia ya marehemu Mbwana Masoud, Ndugu Jamaa na Marafiki wa familia yake na kwa kuwa kijana huyo alikuwa Wakala wa Chadema, pia CCM inapenda kutoa pole kwa Viongozi na wanachama wa Chadema kufuatia msiba wa kijana huyo.”

Taarifa hiyo imesema pamoja na masikitiko hayo, CCM inakanusha vikali uvumi uliotolewa na baadhi ya watu na kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kwamba Chama Cha Mapinduzi kinahusika na kifo cha kijana huyo.

“Taarifa hizo si za kweli kabisa, na kwamba zimejaa uongo na uzushi, huku zikibeba dhamira ya kuipaka matope CCM mbele ya umma.

“Lazima itambulike kuwa CCM ni chama Cha siasa ambacho kutokana na historia yake, hata siku moja hakijawahi na hakitakuja kuendesha hila chafu kama hizo zinazoweza sababisha mauaji ya mwananchi yeyote, kwa sababu hiyo si sehemu ya kazi ya siasa kinayoifanya.”

CCM inavitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka ili kuwabaini na kuwakamata wote watakaobainika kuhusika na unyama huo ili ukweli dhidi ya mauaji hayo uweze kujulikana mbele ya umma.