CCM yaipa pole Afrika Kusini kwa msiba

Na Mwandishi Wetu

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa pole kwa chama cha ANC,
kufuatia kifo cha Mama Nontsikelelo Sisulu, mke wa aliyekuwa mpigania uhuru wa nchi
ya Afrika Kusini, Walter
Sisulu
.


Akizungumza baada ya kutia
saini kitabu cha maombolezo ya kifo hicho jana Ubalozi wa Afrika Kusini mjini
Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema, CCM
imeguswa na kifo hicho kwani, Mama Sisulu alikuwa mstari wa mbele kupigania
haki na usawa wa binadamu pia.


Nape alisema, katika uhai
wake, Mama Sisulu alitumia taaluma yake ya uuguzi kuwafundisha wauguzi wenzake
ambao walihudumua wanaharakati waliokuwa katika mapambano ya kusaka uhuru wa
Afrika Kusini.


Alisema, Mama sisulu atabaki
kuwa mfano wa wapenda usawa wa binadamu duniani kwa sababu hata baada ya Afrika
Kusini kupata uhuru, alikuwa miongoni mwa viongozi waliosimamia maridhiano ya
kusahau madhila yaliyofanywa baina ya makaburu na raia wa Afrika kusini kabla
ya uhuru.


Nape alisema, licha ya ukatili
na ubaguzi wa rangi waliokuwa wakiufanya makaburu, lakini maelewano
yaliyofanyika baada ya uhuru wa chini ya wanaharakati akiwemo Mama Sisulu
wazungu hawakubaguliwa. Alisema matendo ya Mama Sisulu yatabakia kuwa mfano
bora kwa wapinga ubaguzi na wapenda amani duniani ikiwemo Tanzania.