CCM yaiagiza Serikali kuwalipa madeni wakulima

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilsom Mukama akizungumza na wanahabari.

Na Mwandishi Wetu

HALMASHAURI Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi iliyokutana hivi karibuni imeitaka Serikali kutafuta fedha haraka kwa kuamua kuuza mahindi tani 80,000 kwa UNFP na nchini Kenya ili kulipa madeni ya wakulima.

Aidha imeiagiza Serikali kuhakikisha inanunua mahindi ya wakulima yaliyopo majumbani na kwenye vituo vya ununuzi kabla ya upandaji wa msimu mpya haujaanza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama kwa vyombo vya habari jana, amesema CCM pia imeipongeza Serikali kwa kuruhusu uuzaji wa mahindi nje ya nchi, hali ambayo itasaidia mahindi yaliyobaki kwa wakulima kupata soko.

Hata hivyo, imesisitiza kuwepo na tahadhari sasa na siku zijazo, ili chakula chote kisiuzwe nje ya nchi na kusababisha tatizo la njaa nchini, hivyo kuitaka Serikali iimarishe Wakala wa Chakula wa Taifa kwa kuuwezesha kwa fedha zaidi na kujenga maghala mengi na makubwa zaidi ili uweze kununua kiasi kikubwa cha mazao.

Pamoja na hayo CCM imeiagiza Serikali ihimize kuundwa kwa Vyama vya Ushirika vya Mazao ya Chakula, ambavyo navyo viwezeshwe kujenga maghala ya kuhifadhi nafaka katika maeneo yao pamoja na kuanzisha mfumo wa ununuzi wa mazao wa stakabadhi ghalani.

Kuhusu mjadala wa Katiba mpya Halmashauri Kuu ya Taifa imewataka wananchi na wanachama wa CCM kuelewa, kutambua, na kuamini kwamba Katiba mpya pamoja na mchakato wa kuipata, ni kwa manufaa ya nchi. Imewataka Wabunge na viongozi wengine wa ngazi zote nchi nzima kuwaelewesha wananchi si tu maudhui yake, bali hata faida zake.