CCM yagawanyika Songea

CCM yagawanyika Songea

Na Mwandishi Wetu
Songea

WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinatengeneza mazingira ya kujisafisha kuanzia ngazi ya Taifa hadi kwenye matawi kwa kauli ya kujivua gamba, baadhi ya wanachama Wilaya ya Songea Vijijini wameushutumu uongozi wao kuanza kukigawa chama hicho.

Baadhi ya wanachama hao wamelilalamikia kundi la viongozi wilayani humo kwa kitendo cha kumtelekeza Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo, Ali Madamba baada ya kupata ajali akiwa kazini Aprili 6, mwaka huu akielekea Muhukuru.

Wanachama hao ambao wameomba majina yao kutotajwa kwa kuwa si wasemaji jana waliliambia Jambo Leo mjini hapa, kuwa hali ya kisiasa wilayani Songea Vijijini ni tete kwani viongozi wao wamegawanyika.

Taarifa zilisema viongozi hao wamegawanyiika katika makundi mawili, moja linaongozwa na Katibu wa Wilaya, Lidya Gunda pamoja na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Muhagama na lile la Mwenyekiti wa CCM Wilaya hiyo, Ali Madamba.

Imeelezwa kuwa hali si nzuri ndani ya chama hicho kwani uendeshaji wa shughuli haufuati Sera wala Katiba ya chama zaidi ya mvutano wa makundi hayo ambayo yameanza kukidhoofisha chama wilayani hapo.

Wanachama hao kutoka kata za Mpitimbi, Matimira, Maposeni na Litisha wameuomba uongozi wa CCM Mkoa wa Ruvuma kuchukua hatua za haraka kuangalia mpasuko huo ili kuninusuru chama chao.

Mgawanyiko huo unadaiwa kuvuma zaidi baada ya kiongozi mmoja (Mbumge wa CCM) kutaka uongozi wa wilaya hiyo kuanza kujivua gamba mapema na wasitupie mzigo huo kwa watendaji wa chini.

“Sasa imefikia hatua kuanza kufukuzana ndani ya chama bila kufuata utaratibu jambo ambalo limeanza kuleta hofu kwa wanachama…mfano wameanza kufukuzana wenyewe bila utaratibu,” kilisema chanzo kimoja.

Imeelezwa kuwa Aprili 6, mwaka huu, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini, Madamba baada ya kupata ajali aliomba usafiri wa kumtoa Muhukuru hadi Hospitali ya Misheni ya Peramiho Katibu wa Wilaya hiyo, Gunda alidai gari halina mafuta, hivyo kupewa msaada na gari la wagonjwa.

Madamba amekiri kuwa tangu apate ajali Gunda pamoja na viongozi wenzake akiwemo Mbunge wa Peramiho hawajamtembelea kumjulia hali jambo ambalo linaonesha kuna mgawanyiko katika uongozi wa Wilaya hiyo.

Hata hivyo Muhagama alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo alisema wakati Madamba anapata ajali alikuwa bungeni Dodoma na kuongeza malalamiko hayo ni ya upande mmoja kwani Madamba naye hakufika msibani yeye alipofiwa na mumewe.

Jitihada za kumpata Gunda hazikufanikiwa, japokuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma, Emmanuel Mteming’ombe kuwepo kwa mgogoro baina ya Gunda na Madamba na wameanza kusuruhisha.