CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimejibu hoja zilizoelekezwa kwao na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hivi karibuni baada ya kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichomalizika hivi karibuni.
Wakijibu hoja hizo, CCM imesema kwamba isingependa kufanya majibizano na CHADEMA kwa kuwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi wana kazi nyingi za kufanya kutekeleza ilani ya chama ilhali CHADEMA hawana cha kufanya zaidi ya kuandamana.
Katika kauli hiyo ya CCM iliyotumwa kwa vyombo vya habari jana, na kusainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Itikadi na Uenezi, John Chiligati inasema, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe (Mb) na chama chake anapotosha umma juu ya kauli anazotoa dhidi ya CCM.
“Maazimio ya kikao hicho (cha CHADEMA)…baadhi yanapotosha umma kwa kiwango kikubwa,…CCM isingependa kuendeleza malumbano na CHADEMA kwa vile kama chama kilichopata ridhaa ya wananchi kuongoza Taifa, kinayo kazi ya kutekeleza ahadi zilizomo katika Ilani yetu ya Uchaguzi, na si kupoteza muda kulumbana na CHADEMA ambao hawana kazi ila ni kuandamana nchi nzima na kutoa maneno ya kuwafitinisha wananchi dhidi ya Serikali,” alisema Chiligati.
“CCM tusipo jibu hoja za upotoshaji za CHADEMA wananchi wanaweza kuamini upotoshaji huo kuwa ni ukweli,” alisema Chiligati katika taarifa yake.
Aidha akizungumzia hoja ya CHADEMA ya kuishinikiza Serikali ya CCM kutoilipa kampuni ya Dowans sh. bilioni 94 ambazo zimezua mvutano, alisema suala hilo tayari Kamati Kuu ya CCM, ikiungwa mkono na Kamati ya Wabunge wa chama hicho iliiagiza Serikali isiilipe Dowans kwa kuwa kuna kesi Mahakama Kuu ya Tanzania inayopinga malipo hayo.
Alisema kitendo cha CHADEMA kudai inaishinikiza Serikali isilipe deni hilo ilhali Mahakama Kuu haijatoa uamuzi wowote ni sawa na kudanganya umma.
“Tunapenda wananchi waelewe kwamba suala hili lipo Mahakama Kuu kwa lengo la kutafuta nafuu kuhusu deni hili…,” alisema Chiligati.
Hata hivyo, akizungumzia hoja ya CHADEMA kwamba inaishinikiza Serikali kushughulikia tatizo la mgawo wa umeme na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, alisema Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya Februari, 2011 alitoa ufafanuzi wa kutosha.
Chiligati alisema, ukame ndiyo uliosababisha maji kupungua katika bwawa la Mtera ambalo ndilo muhimili wa uzalishaji umeme wa nguvu za maji.
“Rais alieleza hatua za muda mfupi za kuleta majenereta ya kukodi ili kuondoa haraka tatizo hili ambalo linaumiza sana wananchi, uchumi, na huduma mbalimbali. Rais alieleza hatua za muda wa kati na muda mrefu za kupambana na tatizo hili kama vile kuongeza umeme kupitia matumizi ya gesi ya Mnazibay Mtwara na Songosongo, kuzalisha umeme kupitia nguvu ya upepo (Mradi wa Singida)…,”.
Aidha kuhusu upandaji bei za bidhaa mbalimbali, alisema chimbuko ni kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hali iliyosababishwa na machafuko ya kisiasa katika nchi za Uarabuni zinazotoa mafuta kwa wingi na tayari Serikali imeanza kupambana na wafanyabiashara wa Sukari ili bei ya bidhaa hii ishuke.
Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa Meya wa Arusha na kuzua mvutano, alisema ulifanyika na kukamilika kwa mujibu wa Sheria, hivyo Mahakama ndio chombo kinachoweza kubatilisha matokeo ya uchaguzi na si kwa maandamano.
“Njia ya kuchochea watu wafanye vurugu kwa kisingizio cha kupinga mchakato wa uchaguzi wa umeya, si njia sahihi na CHADEMA waelewe kwamba watabeba lawama zote za matokeo ya vurugu hizo,” alisema Chiligati katika taarifa hiyo.
Mwisho.