MKOA maalum wa vyuo vikuu, kanda ya Dar es salaam, umefanya kikao cha kujadili mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha Mkoa huo na Chama kwa ujumla.
Pamoja na Ajenda hiyo, pia kikao hicho:-
• Kimelaani vikali matukio ya kuvamiwa, kudhuru mwili na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa Dini na wanahabari. Mkoa umesikitishwa sana na tukio la kushambuliwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006 Ndugu Absalom Kibanda.
• Lakini pia, kimevitaka vyombo vya Dola kuwakamata, kuwashikilia na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliothibitika kuhusika na matukio ya namna hiyo bila kuangalia Itikadi za Kivyama, Cheo ama Kundi. Na pia kuyataka makundi ya kijamii, wanaharakati na wanasiasa kuacha kuingilia/kuvuruga kwa namna yeyote taratibu za kisheria na kiusalama.
• Pia, kuwataka wanausalama kumhoji kwa kina Dr Slaa juu ya tuhuma zake dhidi ya Kurugenzi ya Usalama wa Taifa (TISS) na kumtaka kuthibitisha madai yake kuwa baadhi ya watendaji wa taasisi hiyo muhimu na nyeti wanaripoti kwake kinyume cha utaratibu, kanuni na maadili ya taasisi hiyo.
Kwani tuhuma hizo ambazo Dr Slaa amekuwa akizisema mara kwa mara tangu kipindi cha Kampeni za Urais Mwaka 2010 zimeanza kuaminika, lakini pia zimepelekea wananchi sasa kukosa imani na Taasisi hiyo na zaidi kupoteza imani juu ya uwezo wa serikali kuwalinda na kuwahakikishia Usalama wa maisha yao, ambapo ni jukumu la kikatiba la serikali.