CCM Sasa Kuijadili Rasimu ya Katiba Ndani ya Chama

Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa habari leo

KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imekutana Juni 10, 2013 chini ya uenyekiti wa Mwenyekiti wa Taifa wa CCM Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye baada ya kikao cha siku moja na maalum kwa ajili ya kupokea rasimu ya katiba mpya, Kamati Kuu imeipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini kwa kazi nzuri na kukamilisha kazi kwa wakati.

Nnauye amesema Kamati Kuu imeagiza rasimu ipelekwe kujadiliwa tena ndani ya chama na wananchi kwa kuwa, bado pia wananchi kupitia mabaraza mbalimbali ya katiba yataijadili.

“Kamati Kuu imekiagiza Chama kijipange kuijadili rasimu hiyo ndani ya Chama kama baraza la kitaasisi la katiba na kuwataka wanachama na wapenzi wa CCM wajitokeze kwa wingi na kushiriki kwenye mabaraza hayo.”

“Ushiriki huu wa CCM baada ya kupokea rasimu umekusudia kushirikisha wanachama wake kwenye ngazi ya matawi, wilaya, mkoa na Taifa. Lakini pia Jumuiya za CCM zimekusudia kushiriki kama mabaraza ya Katiba na hivyo kuongeza ushiriki wa wanachama na wapenzi wa CCM katika mchakato huu,” alisema Nnauye katika taarifa yake.

Aliongeza kuwa CCM kama baraza la katiba la kitaasisi litaipitia rasimu iliyowasilishwa kifungu kwa kifungu na kwa kuzingatia maoni ya CCM yaliyotolewa mwanzoni kabisa mwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba na wanachama watashirikishwa.

“Pamoja na kazi nzuri ya Tume ya Mabadiliko ya katiba, Kamati Kuu inaiomba Tume hiyo kueleza vizuri mchakato mzima kutoka rasimu ya kwanza mpaka rasimu ya mwisho ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi juu ya mchakato mzima hasa baada ya rasimu ya kwanza kutoka.”

“Kamati Kuu inawasihi Watanzania kushiriki tena kwenye kutoa maoni kupitia mabaraza ya katiba kwa rasimu ya kwanza, bunge maalum la katiba kwa rasimu ya pili na kupitia kura ya maoni kwa rasimu ya tatu, kwa amani,utulivu na kuvumiliana ili mwisho wa siku tupate Katiba nzuri ya nchi yetu kwa masilahi ya Watanzania walio wengi.” Imesema hivyo taarifa ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.