CCM Kurejesha Imani ya Chama, Kuwaengua Walioingia kwa Rushwa Madarakani

Rais Jakaya Kikwete akihutubia wanachama na wapenzi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano huo. Picha na Ikulu.

Na Mwandishi wa dev.kisakuzi.com

SEKRETARIETI
mpya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyoingia madarakani hivi karibuni chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, imesema itahakikisha vitendo vya rushwa hasa kwenye chaguzi za chama hicho vinakoma mara moja, tofauti na ilivyokuwa imezoeleka.
Kauli hiyo ya viongozi wa juu wa CCM, Mwenyekiti Taifa (Rais Kikwete), Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara (Phillip Mangula) na Katibu Mkuu (Abdulrahman Kinana) imetolewa leo na viongozi hao wakati wakizungumza na wana-CCM Mkoa wa Dar es Salaam katika mkutano wa kumpongeza Rais Kikwete kuchaguliwa kushika nafasi hiyo tena.
Akizungumza na umati wa wanachama hao, Rais Kikwete aliwataka viongozi wapya kufanya kazi ya ziada ya kuhakikisha wanarejesha imani ya Watanzania kwa CCM, ambayo haiko kama ilivyokuwa zamani.
“Lazima kujiuliza nini kimekifanya chama hiki kufikia hapo kilipo na kuangalia nini cha kufanya ili kuondokana na hali hiyo. Pale mnapohisi hali ya kuungwa mkono inapungua lazima tujiulize, kulikoni..! Nini cha kufanya ili kuimarisha chama,” alisema na kuongeza kuwa kazi nyingine ni kuhakikisha wanakijenga chama na kuimarisha zaidi ili kiendelee kuwaongoza Watanzania.
“Chama chetu hakifanyi mikutano…wenzetu wanafanya kwanini sisi hatufanyi, sasa tutatengeneza utaratibu maalumu kuhakikisha viongozi wa chama kwa nafasi zao wanafanya kazi yao ipasavyo ndani na nje ya chama,” alisema Rais Kikwete.

Alisema ipo haja ya kujipanga na kuangalia namna ya kupambana na propaganda hasi za baadhi ya vyombo vya habari na wapinzani ili kukabiliana na hali hiyo. Aliwataka wanaCCM kuacha makundi na chuki ambayo yamekuwa yakikigawa chama hicho.

Awali akizungumza Kinana alisema vitendo vya rushwa ndani ya CCM watahakikisha vinakoma mara moja ili kurejesha imani ya Watanzania iliyopungua kutokana na tuhuma za wachache dhidi ya vitendo viovu.
Alisema chini ya uongozi wake atahakikisha mashaka yaliotawala kwa wananchi dhidi ya CCM yanaondoka kwa kuwaengua wale wanaoendeleza vitendo vya rushwa, majumbu na vitendo vinavyo leta sifa mbaya ya chama hicho.
“Hatuwezi kuiongoza nchi yetu wakati watu wanamashaka na sisi, lazima tuondoe mashaka akisimama mwana-CCM wote waseme naam huyu anaweza kusema…sio akisimama mwana-CCM kusema watu wanahoji haaah, na huyu naye anakemea rushwa?
Aliwataka wana-CCM kushirikiana katika kukisafisha chama na si kuwaachia viongozi jukumu hilo, ambalo wao kama viongozi wamekubali kuongoza mapambano hayo.

Alisema CCM ina wanachama milioni 5 ambao asilimia 99.9 wengi wakiwa ni masikini na waadilifu huku asilimia 0.1 wakiwa ni wala rushwa wakubwa, wapenda mizengwe, wapendeleaji hivyo kujikuta idadi hiyo ikikichafua chama chote jambo ambalo alisema chini ya uongozi wao hawawezi kuacha hali hiyo iendelee.
Alisema atahakikisha anasimamia ilani ya chama vizuri huku kanuni mbalimbali zikifuatwa ili kuleta haki ndani ya chama hicho, alisema kuna kazi kubwa ya kukijenga chama hicho,
Alisema pamoja na viongozi wenzake watahakikisha baadhi ya wana-CCM waliokuwa na tabia za mizengwe pamoja na kupanga safu za viongoli ili kubebana kimaslahi inatoweka, hivyo kumtaka kila mwanachama afanye kazi ya kumuingizia kipato na si kutegemea kunufaika na nafasi ya uongozi.
Naye Makamu Mwenyekiti Bara, Mangula alisema wapo baadhi ya viongozi wameingia ndani ya chama kwa rushwa na tayari malalamiko juu ya mizengwe ya uchaguzi wa chama hicho uliofanyika yamewafikia, hivyo kwa sasa wataanza kupitia kwa kina kila malalamiko na atayebainika kuingia kwa rushwa ataenguliwa bila kumuogopa.
“Tunajipa miezi sita ndani ya miezi sita walioingia kihalali wataendelea lakini walioingia hovyo hovyo ‘out’…walioingia kwa pesa nje, hata wale waliokuwa wanatumwa vibahasha nao tukiwajua wale nje, hatukubali chama chetu kituhumiwe kwa rushwa, wala hatuta ngoja ushahidi sijui wa TAKUKURU, Polisi hakuna tutakisafisha Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
“…Lakini na nyingi mliokubali kununuliwa kama sambusa mlifanya makosa, tusikubali tena…kwanini mtu ukubali kuthaminishwa kama sambusa?,”