Na Joachim Mushi, Longido
MGOMBEA Mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu amesema endapo cham hicho kitafanikiwa kuingia madarakani watamaliza shida ya maji katika Jimbo la Longido na Hanang. Samia ametoa ahadi hiyo leo mjini Longido alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara akiinadi ilani ya CCM katika uchaguzi mkuu utakao fanyika Oktoba 2015.
Alisema katika ilani ya CCM imepanga kutumia shilingi bilioni 13 kutoa maji eneo la Simba kwenda Longido pamoja na mji wa Namanga, mradi ambao mgombea huyo mwenza ameahidi utatekelezwa mara moja Chama Cha Mapinduzi kitakapo fanikiwa kupewa ridhaa ya kushika dola Oktoba 25, 2015.
Bi. Samia alitoa ufafanuzi huo baada ya mbunge anaemaliza muda wake Lekule Laizer kumuomba asaidie kuwatatulia kero ya maji, vibali vya biashara mpaka wa Namanga pamoja na mpangilio wa makazi katika Mji wa Longido. Alisema ilani ya Serikali itakayoundwa na CCM imepanga kusimamia mradi wa maji Longido ili kumaliza kero hiyo kwa wananchi hivyo kuomba waichague CCM uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2015.
“…Suala la maji tumepanga kutumia fedha shilingi bilioni 13 kutoa maji Simba kwenda Longido na Namanga, mradi ambao Serikali ya CCM itaukamilisha mapema tutakapoingia madarakani. Nimesikia hapa mpakani mna tatizo la upatikanaji vibali vya kufanya biashara…hili niseme kwamba Serikali ya CCM ilani yake imekemea kabisa suala la kuwabughudhi wafanyabiashara hasa wanaoanzisha biashara zao, mtakapotupa nafasi hili tunawahakikishia litamalizika,” alisema Bi. Samia Suluhu.
Aliongeza kuwa ilani ya CCM imepanga kuboresha huduma za kijamii zikiwemo afya, elimu na upatikanaji huduma za maji safi na salama. Alisema Serikali ya CCM imepanga kujenga hospitali ya Wilaya Longido ili kutoa huduma bora za afya kwa wananchi pamoja na kusimamia asilimia tano ya fedha kutoka halmashauri ili ziweze kuwasaidia vijana na akinamama katika vikundi.
Kwa upande wake mbunge Laizer aliwataka wananchi kuichagua CCM ili iweze kufanya mambo mazuri iliyoyaanzisha katika Wilaya hiyo mpya ya Longido. Alisema Jimbo la Longido ni ngome ya CCM hivyo wananchi wanajua mengi mazuri yaliyofanywa na serikali ya CCM ikiwa madarakani hivyo lazima wataichagua tena.
Alisema Wilayani Longido hawajutii kitendo cha Edward Lowassa kukikimbia chama kwani hakuna kitu cha maana alichofanya ndani ya jimbo hilo kitakachowafanya kumkumbuka zaidi ya kuwakandamiza kibabe wananchi wa eneo hilo hasa wakati wakiomba kupewa kuwa wilaya. “…Mimi sioni chochote cha maana ambacho amefanya hadi tusikitike au kujutia kuondoka CCM, na wala hatuwezi kumfuata maana kila mtu aliingia CCM mwenyewe na ataondoka mwenyewe,” alisema Laizer.
Mbunge huyo anayemaliza muda wake aliwaomba wananchi kumchagua mgombea ubunge aliyemuachia nafasi hiyo Dk. Steven Lemomo anayegombea Jimbo la Longido kwa sasa, ambapo aliahidi kumtembeza vijiji vyote vya jimbo hilo na kumweleza kero zilizopo ili aweze kuzimalizia. Bi. Samia Suluhu alifanya mikutano mitatu katika maeneo ya Namanga, Longido na Monduli.