BAADHI ya wenyeviti wa mikoa wamesema kura za maoni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na mchakato wa kujivua gamba, ndiyo umekuwa ukitesa chama hicho kikongwe barani Afrika. Wiki iliyopita, kada mwandamizi wa chama hicho na mlezi wake mkoani Arusha, Stephen Wassira alikuwa akihaha kusaka suluhu ya mpasuko ndani ya Umoja wa Vijana (UVCCM) na wa CCM ndani ya mkoa huo.
Jana, ilikuwa ni zamu ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa ambaye aliongoza kikao cha kupokea taarifa ya hali ya kisiasa na amani ndani ya chama hicho kutoka kwa wenyeviti wa mikoa 26 ya Tanzania Bara na Visiwani.
Katika kikao hicho, taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinasema kwamba kujivua gamba kwa CCM na mchakato wa kura za maoni za mwaka jana, ndiyo majeraha makuu yanayokitafuna chama hicho katika mikoa 21 ya Tanzania bara.
Akizungumza baada ya mapumziko ya mchana, Msekwa alikiri mambo hayo kutawala kikao hicho na kusema: “Tunachofanya hapa ni kupokea taarifa. Hiki siyo kikao cha uamuzi, tunapokea taarifa ya hali halisi ya kisiasa ndani ya chama kwa mikoa yote ya bara na visiwani.”
“Ni vikao vinavyofanyika mara kwa mara, lakini safari hii mimi ndiyo nipo naongoza nikichukua nafasi ya mwenyekiti wa taifa ambaye ni Rais. Yeye yuko nje, sasa tumeona ni vyema niwepo hapa kusimamia na kusikiliza taarifa za wenyeviti wa mikoa yote.”
Gamba
Akizungumzia kujivua gamba, Msekwa alisema baadhi wanahoji kwa nini jambo hilo haliendi kwa kasi kulikamilisha ili hatua hiyo iweze kufika pia ngazi ya chini.
Makamu huyo alisema uamuzi huo wa kujisafisha ni wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec), lakini akatoa angalizo: “Tunachofanya sasa katika kutekeleza hili ni kitu kinachoitwa ‘political management’ (menejimenti ya siasa). Hatuwezi kufanya jambo hili kwa shinikizo.”
Alisema CCM ni chama cha siasa ambacho kinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu zote za kiuongozi hivyo, hata utekelezaji wa uamuzi wake unapaswa kusukumwa kwa kanuni na misingi ya uongozi wa chama cha kisiasa na si vinginevyo.
“Ni kweli tunajua hili linapaswa kutekelezwa, lakini tukianza kufanya mambo bila utaratibu itakuwa tatizo. Wapo wanaosema labda dhana hii haijaeleweka kwani haimaanishi wanaopaswa kuwajibika au kujiuzulu ni watu wa ngazi za juu tu kama sisi labda,” alisema.
Katika hilo la kujisafisha Msekwa alisema: “Ndiyo hivyo tunasema tunahitaji kufanya haya yote kwa kufuata ‘political management’. Maana tunataka kusafisha chama hadi ngazi za chini.”
Alisema katika kutekeleza azma hiyo kwa kutumia taratibu hizo za menejimenti ya siasa, ni vigumu kusema mchakato huo wa kusafisha chama kwa watu wasio na maadili kuwajibika, utakamilika lini.
Mpango wa CCM kujihuisha kwa kujivua gamba, ulitangazwa na Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete katika maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa chama hicho baada ya kukiri kwamba kuna watu wanaokichafua ambao watapaswa kuachwa mbele ya safari au wenyewe wajiengue.
Baada ya kauli hiyo, Nec iliazimia watu wote waliotajwa katika tuhuma mbalimbali zikiwamo za wizi katika Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambao wanahusika na Kampuni ya Kagoda wawajibike na wengine waliohusika na mkataba wa kifisadi wa Richmond na kashfa ya rada.
Utekelezaji huo ulipaswa kufanyika ndani ya siku 90, lakini hadi sasa haujafanyika huku kukiwa hakuna dalili zozote za wahusika kuwajibika wenyewe au kuwajibishwa na chama kupitia vikao vyake vya uamuzi.
Kura za maoni
Kuhusu kura za maoni, Msekwa alikiri wenyeviti wengi kuulalamika kuwa ulichangia mpasuko na mchezo mchafu wa kufyatuliwa kadi bandia kwa wanachama hivyo kusababisha manung’uniko kwa walioshindwa.
Alisema wenyeviti wengi walieleza katika taarifa zao za awali kwamba kura hizo zilisababisha wale walioshindwa katika baadhi ya maeneo, kutokubali matokeo na kuanza kujenga uadui na uhasama ambao umekuwa ukisababisha matatizo katika chama ngazi ya mikoa.
Msekwa alisema katika hilo chama kinaangalia namna ya kurekebisha kasoro hiyo ili katika mchakato wa kupata wagombea kwenye uchaguzi ujao ili kuendeleza umoja na mshikamano ndani ya chama.
Makamu mwenyekiti huyo wa CCM alisema baadhi ya wenyeviti walilalamikia agizo la dakika za mwisho la aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba kuagiza wote wenye kadi za chama hicho kupiga kura hatua ambayo ilichangia kuwapo kadi nyingi bandia.
Hata hivyo, Msekwa alisema baada ya kupata taarifa kutoka kila mkoa chama kitajitathmini kwani taarifa hizo zitasaidia katika kuangalia upungufu na uimara na namna ya kurejesha umoja, amani na mshikamano.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinadai kwamba mikoa ambayo inaonekana kutafunwa na siasa za gamba ni Dar es Salaam, Arusha, Shinyanga, Mara na Tabora ambako kumekuwa na misimamo tofauti ya viongozi kuhusu dhana hiyo.
Hadi jana, baadhi ya mikoa hiyo yenye msuguano wa siasa za gamba, wenyeviti wake walikuwa hawajawasilisha taarifa zao za hali ya siasa na amani. Kikao hicho cha siku moja, pia kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mkama na maofisa wengine waandamizi.
CHANZO; Mwananchi