CCM inatekwa na matajiri – Sumaye


Fredrick Sumaye

Moshi
WAZIRI Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Fedrick Sumaye amesema zipo ishara ambazo zinajitokeza ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambazo kama hazitaangaliwa vizuri zitakivuruga chama hicho na nchi kwa jumla.
Sumaye aliyasema hayo jana akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Pasua, Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, ambapo alisema moja ya ishara hizo ni kuwepo kwa dalili za chama kutekwa na watu wachache wenye fedha na kusahau jukumu la msingi la kutetea wanyonge.
Alisema mwelekeo huo ni hatari kwa chama na mstakabali wa Taifa kwani sasa nchi inaitegemea CCM, hivyo lazima chama hicho kikae katika misingi inayoeleweka.
Alisema nia yake si kuwapiga vita wala kuwachukia matajiri, kwani chama kinawapenda sana lakini wasikiteke nyara chama, kwa kuwa lazima kibaki kama chama cha kuwatetea wanyonge na nchi kwa dhati.
“Yapo maeneo ambayo CCM tunatakiwa tuyaangalie kwa umakini mkubwa kwani ipo dalili ya chama chetu kutekwa na watu wachache wenye fedha na mwelekeo huu ni hatari sana ndani ya chama na taifa kwa ujumla na kama hatutakuwa makini hali hii inaweza kukivuruga chama,” alisema Sumaye.
Aidha alisema Jambo lingine ambalo linapaswa kuangaliwa na chama hicho ni amani na utulivu wa nchi kutokana na kwamba zipo dalili ambazo zinaonyesha kutikisika kwa msingi huo wa amani na utulivu katika nchi.
Alisema yapo mambo ambayo yameanzakujitokeza ikiwemo harakati za kisiasa kwani nchi ipo katika mfumo wa vyama vingi vya kisiasa na lengo la mfumo huo ni kuimarisha misingi ya demokrasia ili watu wawe na uhuru wa kuchagua mawazo ambayo wanataka kuyasikia na wala nchi haikuingia katika mfumo huo ili kujenga chuki na kupigana mawe.
Alisema chama cha siasa ambacho kinataka kuiongoza nchi hakitakiwi kiwe na fujo kwani hata chenyewe hakitaweza kutawala kwenye fujo na fujo ikishaanzishwa nchini hazitakoma.
“Naniomba sana tuwe waangalifu na midomo yetu, matendo yetu na kuhusu mambo ya siasa,na mfumo wa vyama vingi usitugawe bali utuimarishe na utupe upendo zaidi,” alisema Sumaye.
Hata hivyo Sumaye alikitahadharisha chama hicho na ufisadi na udhalimu kwa kusema kuwa hali hiyo kwa sasa inazidi kukua kwa kasi na kuota mizizi hali ambayo kama haitaangaliwa itakifikisha chama mahali pabaya.
Alisema chama hicho kwa sasa hakitakubali mtu yeyote kukivuruga bali kitaendelea kujisafisha na kuhakikisha kuwa wanachama wote wanakuwa safi.
Alisema ili kuweza kushinda vita ya ufisadi nchini ni lazima CCM wenyewe waanze kwanza kujivua magamba yao hata kama inaumiza ndipo waweze kupiga vita ufisadi.
Sumaye akizungumzia suala la Muungano alisema muungano kwa sasa umedumu kwa miaka 47 na uko imara hivyo wananchi wasilogwe wakaubeza muungano huo.
Alisema kwa sasa ukilisikiliza mijadala katika bunge na baraza la wawakilishi inaonyesha wazi kuwa kuna haja ya kuuzungumzia muungano kwa maslahi ya watanzania wote hasa katika wakati huu ambao kuna mjadala wa katiba mpya na lengo liwe kuuimarisha na wala si kuuvunja.