Na Joachim Mushi, Dar es Salaam
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) imesema itashinda Uchaguzi Mkuu mchana kweupeee hapo Oktoba 2015 licha ya aliyekuwa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa na kada nguli wa chama hicho kukihama na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana.
CCM imetoa kauli hiyo leo ilipokuwa ikizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku moja tu baada ya Lowassa kujiondoa mwenyewe ndani ya chama hicho kwa madai hakikumtendea haki katika mchakato wa kumteuwa mgombea urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho.
Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM, Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Simba alisema chama hicho hakiwezi kutetereka kwa kuondoka mwanachama mmoja kama Lowassa kwani hajaanza yeye kutoka na kuingia katika chama hicho. Alitolea mfano wapo viongozi waliokuwa na wafuasi wengi ndani ya CCM kama Augustine Mrema lakini aliondoka na chama hicho kiliendelea kudumu na kufanya vizuri miaka yote.
“…Nani anamkumbuka enzi za Augustine Mrema alikuwa akisukumwa kwenye gari na wafuasi wengi lakini aliondoka na CCM ilibaki palepale…CCM haitegemei mwanachama mmoja, nakuakikishia kuwa tutashi uchaguzi mchana kweupeee we subiri,” alisema Simba.
Alisema anashangaa CHADEMA kumpokea Lowassa wakati walikuwa wakimsema vibaya kila kukicha katika mikutano yao ya hadhara. Aliongeza CCM haiwezi kuingilia uamuzi wa Lowassa alipenda kuingia mwenyewe CCM na ametoka mwenyewe kwa ridhaa yake hivyo hawalaumu.
Aidha katika hatua nyingine CCM imeiomba Tume Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) kuongeza mashine na watendaji kwenye vituo mbalimbali vya kujiandikishia wapiga kura ili wakazi wote wanaostahili kujiandikisha kwenye daftari hilo wapate fursa hiyo. Alisema Dar es Salaam ina wakazi wengi takribani milioni tano hivyo kuna kila sababu ya kuongeza vifaa na watendaji kusaidia zoezi hilo.
Aliongeza kuwa wakazi wa Dar es Salaam pia wanatakiwa kutumia fursa hiyo kujiandikisha ili waweze kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Mwezi Oktoba 2015. “…Tunaomba wananchi wajitokeze kujiandikisha kwenye vituo vya kujiandikisha vilivyopo maeneo mbalimbali ya jiji,” alisema Simba.