Chama cha Mapinduzi (CCM) kimempuuza Mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda, kufuatia kauli yake ya kudai kuwa atagombea urais kupitia Chadema katika uchaguzi mkuu wa 2015 na kwamba meneja kampeni wake atakuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Jakaya Kikwete.
Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Wilson Mukama, akizungumza katika mahojiano na NIPASHE Jumamosi jana iliyotaka kujua chama hicho kimepokeaje kauli ya mbunge huyo wa chama cha upinzania kutaka meneja kampeni wake awe Mwenyekiti wa CCM Taifa, alisema Shibuda alikuwa anafanya utani wakati wa kutoa tamko hilo.
“Shibuda alikuwa anafanya utani tu kwa hiyo CCM hatulichukulii kama ni jambo ambalo ni la ‘serious’,” alisema Mukama kwa kifupi na kukata simu.
Mapema Jumatatu wiki hii Shibuda alitangaza azma yake ya kutaka kugombea urais mwaka 2015 mbele ya wajumbe wa NEC ya CCM kwenye semina iliyofanyika Dodoma iliyojadili hali ya utawala bora nchini iliyotolewa na APRM.
Shibuda ni mjumbe wa Bodi ya Taasisi hiyo anayewakilisha vyama vya upinzani.“Nakupa pole, kazi ya urais ni ngumu sana, bila shaka utakumbuka kuwa nami nilitaka kuwa mbadala wako, hata hivyo naamini utakuwa meneja wangu wa kampeni za urais mwaka 2015,” alisema Shibuda akimweleza Rais Kikwete.
Huku wajumbe wa NEC wakishangilia, Rais Kikwete alimwuliza: “Unataka urais kupitia chama gani?” Shibuda akajibu kwa kujiamini: “Kupitia Chadema, huku niliko sasa.”
Hatua hiyo ya Shibuda kutangaza nia yake kugombea urais kupitia Chadema tayari imeleta mashambulizi dhidi yake ambapo Baraza la Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema (Bavicha), limemjia juu mbunge huyo .
Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, John Heche, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari amewataka vijana wote wa Chadema kukabiliana na Shibuda kwa madai kwamba ameonekana kuwa ni kikwazo kwa chama hicho katika kuelekea kuchukua dola katika Uchaguzi Mkuu ujao.
“Natoa wito kwa vijana wote wa Chadema kuwa sasa tujiandae kikamilifu katika kukabiliana na mtu yeyote yule ambaye ataonekana kuwa kikwazo kwa chama chetu, matumaini na maslahi ya Watanzania kwa ujumla wake katika kuelekea kuchukua dola mwaka 2015,” Bavicha imesema kupitia tamko lililosambazwa kwa vyombo vya habari kupitia mtandao wa kompyuta jana.
Heche alisema wamepokea kwa mshituko mkubwa kauli ya Shibuda hasa kutokana na kuitoa kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alitaja sababu za kupokea kwa mshituko kauli hiyo ya Shibuda kuwa ni pamoja na kumtangaza Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kuwa ndiye atakayekuwa meneja wa kampeni zake katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania urais.
Sababu nyingine ni kwa kutamka kwamba hakuna chama kingine chenye uwezo wa kuiongoza nchi kwa sasa na kutoa matamshi hayo kwa niaba ya Mpango wa Bara la Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
CHANZO: NIPASHE