CCM, Chadema sasa ‘vita’ rasmi

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye, akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) jana Dar es Salaam

Dar na Arusha

VYAMA vya CCM na Chadema vimetangaza rasmi vita ya kuwania Ubunge Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha huku vikianika majina ya makada watakaoongoza mapambano kwa ajili ya kujihakikishia ushindi.

CCM ambayo imempitisha Siyoi Sumari kuwania nafasi hiyo, imesema kampeni zake zitazinduliwa na Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho ambaye pia alikuwa Rais wa awamu tatu, Benjamin Mkapa na Chadema itawatumia viongozi wake wa kitaifa, wakiongozwa na Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.

Wakati huo huo, Kamati Kuu (CC) ya Chadema jana ilimpitisha, Joshua Nasari kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Mbowe aliwaeleza viongozi wakuu wa chama hicho, wapenzi na wafuasi wa Chadema waliojazana eneo la Hoteli The Ice Age Usa-River, wilayani Arumeru jana kuwa wamejiandaa kikamilifu kunyakua jimbo hilo na kamwe hawatakubali hujuma zozote kutoka kwa mtu au chama chochote.

Sioi Sumari (wa tatu kulia) akiwa na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Arumeru alipopita Ofisi ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam jana muda mfupi baada ya CCM kumtangaza kuwa mgombea wake baada ya uamuzi wa Kamati Kuu.


Mbowe aliyezungumza kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wake, Dk Slaa kumtanga rasmi Nasari, alitamba kuwa mchakato wa kumtafuta mgombea kupitia chama hicho haujaacha nyufa wala mifarakano miongoni mwa wagombea na wafuasi wao kama ilivyotokea kwa vyama vingine vya siasa ambavyo hakuvitaja.

Alisema mara nyingi mipasuko ndani ya vyama vya siasa hutokana na mchakato wa kupata wagombea kutokana na hila za baadhi ya viongozi, wanachama au wapambe wa wagombea, hali aliyosema haijajitokeza ndani ya Chadema kutokana na mfumo mzuri unaozingatia demokrasia kwa wote bila kujali umaarufu au ukwasi wa mtu.

“Wagombea wote waliojitokeza kuchukua fomu kuomba uteuzi tumewaalika katika Kamati Kuu na wote wameridhika na ushindi na uteuzi wa mgombea mwenzao na wote watashiriki kikamilifu kwenye kampeni kuhakikisha ushindi wa chama unapatikana,” alisema Mbowe.

Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu, Dk Slaa, alisema kikao hicho kilichoshirikisha wabunge, mameya na wenyeviti wa halmashauri za wilaya zinazoongozwa na Chadema, kwa kauli moja kilipitisha jina la Nasari kuitikia sauti ya wananchi na wakazi wa Arumeru waliomchagua kwa kura 805 kati ya 888 zilizopigwa kwenye kura za maoni.

“Wananchi Arumeru tumesikia kauli yenu kupitia kura zenu za maoni, Nasari ni kijana wenu siyo wa Dk Slaa, Mbowe wala Chadema.

Katika kura za maoni, Nasari alimwacha mbali mgombea wenzake Anna Mghiwa aliyemfuatia kwa kupata kura 23 huku wagombea wengine wanne, wakipata kura chini ya 20. Chama hicho pia kinaendelea kufanya tathimini ya kutumia helikopta katika kampeni zake katika jimbo hilo.
CHANZO: Mwananchi, kusoma zaidi habari hii tembelea; www.mwananchi.co.tz