Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), Julius Mcharo akizungumza wakati kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja, ambapo alitumia fursa hiyo kuwashukuru wateja wao kwa kuichagua CBA pamoja na kuwapongeza wafanyakazi wa benki yake kwa kutoa huduma nzuri kwa wateja wao katika mkutano na wanahabari uliofanyika kwenye tawi la CBA Kariakoo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja anayeshughulikia wateja wa CBA Tanzania, Rehema Ngusaru na Afisa viwango na ubora wa huduma CBA Tanzania, Anicetius Buberwa (aliyesimama kushoto).(Picha na Zainul Mzige).
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), Julius Mcharo (aliyekaa kulia) akisikiliza maswali kutoka kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja wa benki ya CBA ambapo watatumia wiki hii kusikiliza nini wateja wao wanataka. Waliosimama kutoka kulia ni Meneja wa tawi la CBA Kariakoo, Vicky Munishi, Boniface Kiwia kutoka makao makuu ya CBA, Tanzania, Rehema Mashayo kutoka makao makuu wa benki ya CBA Tanzania. na kushoto ni Afisa viwango na ubora wa huduma CBA Tanzania, Anicetius Buberwa.
Na Mwandishi Wetu
HUDUMA ya M-PAWA inayotolewa na Benki ya Biashara ya Afrika (CBA) imetoa mikopo ya shilingi milioni 200 katika kipindi cha miezi mitatu tangu ianzishwe. Pamoja na fedha hizo huduma hiyo imewezesha kuwepo na amana za shilingi bilioni 6 kutoka kwa wateja laki 7 ambao wanapata huduma ya M-Pawa.
Taarifa hiyo imetolewa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Julius Mcharo akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya Huduma kwa Wateja iliyofanyika Kariakoo.
Mcharo alisema huduma hiyo inayotolewa kwa ushirikiano kati ya benki hiyo na Vodacom imepata muitikio kutokana na watanzania kuweza kufungua akaunti za huduma hiyo mahali popote pale walipo kwa kutumia mtandao.
Alisema huduma hiyo ambayo pia inawezesha kupatikana kwa mikopo na kupokea na kulipa huduma mbalimbali kwa m-pesa imerahisisha maisha ya wananchi wengi na kusema kwamba itaendelea kuboreshwa na kutanuliwa.
Akizungumzia wiki ya huduma kwa wateja alisema kwamba watendaji wote wa benki hiyo wanakwenda katika matawi yapatayo 11 nchini kote kutoa huduma kwa karibu zaidi na wateja wao kwa lengo la kufahamu changamoto zao.Alisema changamoto hizo zitawawezesha kutambua mahitaji halisi ya wateja na kutengeneza bidhaa zinazolingana na mahitaji yao.
Alisema benki hiyo ambayo ina matawi matano Dar es salaam na mengine yakitawanyika katika miji ya Mtwara, Mbeya,Arusha, Tunduma imejitanua katika kutoa huduma kwa kutumia teknolojia hasa kwa kuwa na huduma za kibenki kwa njia ya mtandao.
Alisema kupitia njia ya mtandao wateja wao wanaweza kupata mikopo na hata kulipa huduma mbalimbali. Aliwashukuru wateja na wafanyakazi kwa kuwezesha ndoto za wengi kutimia kwa kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo na kuwataka waendelee kutumia CBA katika kuchupa mbele kimaendeleo.
Baadhi ya wateja waliohojiwa katika uzinduzi huo walikiri kufurahishwa na huduma za benki hiyo hasa kutokana na kutokuwa na foleni na kujali wateja wao. Charles Mlawa alisema kwamba wamefurahishwa sana na uwapo wa tawi la CBA Kariakoo kwani limefanya waweze kuwa na uhakika na utumaji wa fedha kwa wadau wao ili kupata bidhaa zinazotakiwa.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA), Julius Mcharo akitoa huduma kwa mkazi wa jijini Dar, Bw. Ali Sareva aliyefika kwenye tawi la benki ya CBA lililopo Kariakoo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufungua akaunti ya kampuni yake wakati wa maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja inayoadhimishwa ulimwengu mzima ambapo benki ya CBA wataadhimishi wiki hiyo kwa kusikiliza nini wateja wanachokitaka na kuwa nao karibu zaidi kuboresha huduma zao.
Mlawa alisisitiza kwamba tatizo la usafirishaji fedha nje lilikuwa kero kwao lakini tangu kufika kwa benki hiyo hali ni njema zaidi.Aidha alishukuru kwa huduma nzuri za kibenki zinazotolewa.
Akizungumzia mikopo ya nyumba ambayo benki hiyo ilianza kutoa mwaka 2007 amesema program hiyo inaenda vyema na kwamba hadi sasa wametoa mikopo ya zaidi ya sh bil 25 huku muda wa kulipa ukiwa umeongezwa hadi miaka 20.
Alisema amefurahishwa sana kuwa moja ya mabenki matatu makubwa nchini ambayo yanatoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa makazi.
Meneja anayeshughulikia wateja wa CBA Tanzania, Rehema Ngusaru, amesema kwamba sasa hivi pia kuna mikopo ya kuboresha nyumba.
Aidha amesema kwamba wanahakika ya kuendelea kuwa na huduma nzuri kutokana na mikakati waliyojipangia na kuwakumbusha wafanyakazi namna bora ya kuhudumia wateja.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA) Tanzania, Julius Mcharo (waliosimama wanne kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wateja wa benki ya CBA tawi la Kariakoo pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo kutoka makao makuu ya CBA Tanzania na wafanyakazi wa tawi la Kariakoo.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA) Tanzania, Julius Mcharo akiagana na mmoja wa wateja wa benki hiyo tawi la Kariakoo mara baada ya zoezi la picha ya pamoja.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara ya Afrika (CBA) Tanzania, Julius Mcharo katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzake.