SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya mabadiliko ya mwamuzi wa mechi ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi aliyeondolewa kutokana na sababu za kiufundi ni Jean Claude Birumushahu aliyekuwa mwamuzi msaidizi namba moja. Nafasi yake sasa inachukuliwa na Herve Kakunze pia kutoka Burundi. CAF imemuondoa mwamuzi huyo baada ya kufeli katika mtihani wa waamuzi (Cooper Test) kwa waamuzi wa Burundi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika nchini humo siku tatu zilizopita.
Waamuzi hao na Kamishna wa mechi hiyo Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea wanatarajiwa kuwasili nchini Julai 11 mwaka huu kwa ndege za Kenya Airways na EgyptAir kwa muda tofauti. Nayo Uganda Cranes inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) na itafikia hoteli ya Sapphire. Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) bado halijatuma taarifa rasmi juu ya ujio wa timu hiyo.
Wakati huo huo, makocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na wa Uganda, Milutin Micho pamoja na manahodha wao watakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika keshokutwa (Julai 12 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF kuzungumzia mechi ya Jumamosi.
FRIENDS, POLISI KUCHEZA MECHI YA RCL JUMAPILI
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) imesogezwa mbele kwa siku moja. Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi. Polisi Jamii ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.
Refa Hans Mabena kutoka Tanga ndiye atakayechezesha mechi akisaidiwa na E. Mkumbukwa na Hajj Mwalukuta wote kutoka Tanga. Mwamuzi wa akiba (fourth official) ni Kessy Ngao wa Dar es Salaam. Mechi kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya itachezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Mwamuzi atakuwa Daniel Warioba kutoka Mwanza. Kimondo SC ilishinda mechi ya kwanza bao 1-0.
Boniface Wambura, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)