CAF kutoa leseni za ukucha daraja ‘C’ Tanzania

Ofisa Habari wa TFF, Boniphace Wambura

Na Mwandishi Wetu

KOZI ya ukocha kwa ajili ya kupata leseni za daraja C kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itafanyika Ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanzia Novemba 7 hadi 20 mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema jumla ya makocha 30 wameteuliwa na TFF kwa ajili ya kushiriki kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi wanne, mmoja wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), wawili wa CAF na mmoja wa Chama cha Mpira wa Miguu Denmark (DBU).

Amesema mkufunzi wa FIFA atakuwa Jan Poulsen, kutoka CAF ni Sunday Kayuni (Tanzania), Kasimawo Laloko (Nigeria) wakati kutoka Denmark ni Kim Poulsen. Ameongeza kuwa makocha walioteuliwa kushiriki kozi hiyo ni Christopher Eliakim, Jumanne Ntambi, Keneth Mkapa, Mussa Furutuni, Mecky Maxime, Gideon Kolongo, Maka Mwalwisi, Haji Amir, Tiba Mlesa, Stephen Matata, Wane Mkisi, Edward Hiza, Leonard Jima na Ahmed Mumba.

Wengine ni Peter Mhina, Absolom Mwakyonde, Maarufu Yassin, Mussa Kamtande, Wilfred Kidau, Eliasa Thabit, Dismas Haonga, Fulgence Novatus, Juma Mgunda, Hassan Banyai, Mohamed Tajdin, Sebastian Nkoma, Emmanuel Massawe, Gabriel Gunda, Abdul Nyumba na Richard Kabudi. Pia kutakuwa na kozi nyingine ya juu ya leseni za daraja B ambayo inatarajia kufanyika baadaye Desemba mwaka huu.

Wakati huo huo Mdhamini wa Ligi Kuu ya Vodacom, kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom tayari imeshatoa hundi ya nauli kwa ajili ya klabu ambazo timu zake zinashiriki ligi hiyo. Mgawo uliotolewa ni kwa ajili ya mwezi Septemba na Oktoba.

Tayari klabu husika zimeanza kuchukua hundi zao kutoka TFF. Kwa mwezi Septemba kila klabu imepata sh. 4,732,142 wakati Oktoba ni sh. 5,622,321. Hivyo kwa miezi hiyo miwili kila klabu imepata sh. 10,354,463.

Akizungumzia mapato ya mechi namba 66 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa Oktoba 19 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam imeingiza sh. 14,755,000.

Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 2,794 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 5,000 kwa mzunguko na sh. 10,000 kwa VIP. Waliokata tiketi za VIP walikuwa 157.

Baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,180,763 kila timu ilipata sh. 3,172,271.19. Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 1,057,423.70), TFF (sh. 1,057,423.70), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 528,711.86), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 422,969.49) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 105,742.37).

TFF iko katika mchakato wa kutengeneza mpango wa maendeleo wa muda mrefu. Ni nia ya TFF kufanyia kazi maoni ya wadau ili kuhakikisha yanaingia katika mpango huo.

Hivyo wadau wanakaribishwa kutuma maoni yao kupitia email- tfftz@yahoo.com au sanduku la barua 1574 Dar es Salaam. Maoni yawe yametumwa kufikia mwishoni mwa Novemba mwaka huu.

Pia TFF kupitia Kurugenzi ya Ufundi itakutana na makundi mbalimbali kusikiliza maoni yao. Novemba 2 mwaka huu imepanga kukutana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na pia waandishi wa habari.