Butiku: Serikali iwe sikivu mjadala Katiba mpya

MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku

MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku ameitaka Serikali kuwa sikivu na kusikiliza wananchi wanataka nini juu ya mchakato wa katiba mpya na si wanasiasa na viongozi wa juu kujiamulia watakavyo.

Butiku ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika Kongamano la miaka mitatu ya Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere lililomalizika jana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Umma upewe nafasi ya kutosha kujadiliana na mijadala isiishie kwa wanasiasa na wasomi pekee bali ipelekwe na hata vijijini kwa wananchi wa huko ili nao wachangie. Kama tukifanya hivi tutapata katiba itakayodumu kwa kipindi kirefu na si ilimradi katiba ambayo baada ya muda mfupi tutataka itengenezwe nyingine,” alisema Butiku.

Kwa upande wake Mhadhiri wa UDSM, Prof. Palamagamba Kabudi amewarushia kombora wanafunzi wa chuo hicho na wananchi kwa ujumla kwa kuwataka waache papara na zomeazomea katika mijadala nyeti kama Katiba mpya.

Alisema suala la Katiba ni nyeti, hivyo jambo la msingi ni kwa wananchi wote kushirikiana kutoa mawazo yao yatakayosaidia kupatikana kwa Katiba itakayokidhi matakwa ya umma na kudumu kwa kipnidi kirefu, lakini siyo kuzomeana na kupigana.

“Mwaka 1984 tukiwa wanachuo hapa nilishiriki mijadala ya marekebisho ya Katiba na Mwalimu Nyerere alikuja hapa, Nkuruma tukatoa mapendekezo yetu bila kumtukana wala kuzomeana na Nyerere alisikia mapendekezo yetu na akayafanyia kazi.

Katika hatua nyingine, Prof. Yash Ghai wakati akiwasilisha mada ya Haki za binadamu na Katiba katika nchi za Afrika Mashariki alisema Watanzania wasitegemee kupata katiba itakayokidhi matakwa ya umma kwa kunakili muswada kutoka nchi nyingine.

Prof. Ghai akatumia fursa hiyo kuitaka Serikali kuwapa wananchi muda wa kutosha kujadiliana ni aina gani ya katiba wanaitaka lakini siyo kukimbiza mjadala haraka haraka ilimradi liende.

“Suala la Katiba ni la nchi husika na si kwenda kunakili muswada nchi nyingine na nchi mbili tofauti na kila moja ina mambo yake. Kenya wananchi na wanasiasa walijadiliana kwa muda mrefu mwisho wakapiga kura na hatimaye kupata katiba yao.

“Hivyo na Serikali ya Tanzania inapaswa kuwapa muda mrefu wananchi wajadiliane kwanza kwa pamoja ili waweze kutunga katiba itakayozingatia misingi ya haki za binadamu na haki sawa kwa watu wote na si vinginevyo,” alisema Prof. Ghai.

“Hivyo na nyie vijana na wananchi wengine acheni upapara na zomeazomea zisizo na msingi, tulizeni akili tushirikiane katika kutoa mawazo yetu ni mambo gani tunataka yawemo kwenye katiba yetu, kinyume na hapo hatutafanikiwa,” alionya Prof. Kabudi.

Kongamano la miaka mitatu ya Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere kwa mwaka huu lilianza April 12 na kumalizika jana, ambapo lilijumuisha watu kutoka mataifa mbalimbali ya Kenya, Namibia, Uganda, Eritrea na Afrika Kusini.