Bunge Letu la Katiba Haya Wayazingatie…!
1. Edita nipe nafasi nakuomba kwa hekima
Niseme bila wasiwasi yalo katika mtima
Moyoni yanayonighasi kichwani nikiyapima
Sauti yangu ya kasi ipae dunia nzima
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie.
2. Siyo sauti nyepesi ya mawazo na hekima
Asasi na taasisi twaona vyema kusema
Si bunge la mwendo kasi tunapanga na kupima
Ndiyo tunawasiwasi limebeba yetu dhima
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie.
3. Haki katika afya elimu inayofanana
Hayo kuyapigania na haki kwa wasichana
Yajitokeze sawia na siyo kuyabishana
Nasi twafuatilia na ujumbe kupeana
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie.
4. Tunataka uthubutu yale tuliyoyatuma
Na matarajio yetu hicho ni chombo cha Umma
Yalindwe mawazo kwetu yanayohusu wanawake
Yalogusa Utu wetu na maslahi mazima
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
5. Maadili namba moja agizo tunalitumia
Liende moja kwa moja wanasiasa na vyama
Mkawe kitu kimoja Uzalendo kutazama
Si malumbamo ya hoja kwenye lengo mkahama
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
6. Msirudie ya kale hayo sisi tumegoma
Msifute vipengele vinotusukuma
Mkayatende na yale ambayo tumewatuma
Katiba kama mshale tunahofu kutuchoma
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
7. Na hatutaki Siasa na ushabiki wa vyama
Wakati huu wa sasa mbele tunakutazama
Chombo hiki chatugusa vyema kufika salama
Ama Katiba kipusa nyakati na hizi zama
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
8. Liwe na demokrasia lililojaa hekima
Maoni mkiyatoa na sisi tunayasoma
Kisa tukiyachangia kwenye vyombo mkivuma
Simu tutawapigia na hoja tukizituma
Bunge letu la katiba haya wayazingatie
9. Vyombo vyetu vya habari laivu kutugawia
Katika hiyo safari wote tukashuhudia
Na kufanya tafakari mambo yaende sawia
Katu Dodoma si mbali nasi tukahudhuria
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
10. Na muda uliopangwa huo utumike vyema
Msidai tumezongwa mapesa mmeyafuma
Hilo kwanza linapingwa kutuacha kwenye ngema
Bajeta iliyopangwa ni kodi za wakulima
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
11. Hapa pateni welevu mpawekee nakshi
Nani atoe wasevu kunena na maandishi
Hapa patubana mbovu kulalania hatuishi
Ndugu zetu walemavu kukosa mwakilishi
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
12. Katiba nihatihaki jembe mpini na chuma
Twafuatilia kidhati nyinyi mbele sisi nyuma
Myaguse mambo nyeti Katiba si lele mama
Si kulala kwenye viti jioni bia na nyama
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
13. Ninafanya hitimisho haya yetu masharti
Na wala si vitisho ni sauti ya umati
Hapa nimefika mwisho twaukimbiza wakati
Tamati na ufupisho mimi mwanaharakati
Bunge letu la Katiba haya wayazingatie
Shairi hili limetungwa na Abbas S. Mzeru (Mwanaharakati kutoka GDSS – TGNP – Simu 0713 400759)