*CHADEMA watoa pole kwa familia, wasema ni msiba mkubwa
Na Mwandishi Wetu
BUNGE la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania limetangaza rasmi kifo cha Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Rejia Estelatus Mtema.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo fupi iliyotolewa leo na kusainiwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda, imesema kifo cha Mbunge Mtema kimetokea leo asubuhi mkoani Pwani kwa ajali ya gari.
“Kwa masikitiko makubwa nawatangazia waheshimiwa wabunge na wananchi wote kwamba, Mh. Rejia Estelatus Mtema (Mb), Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amefariki dunia kwa ajali ya gari iliyotokea Jumamosi, Januari 14, 2012 eneo la Ruvu mkoani Pwani,” amesema Makinda.
Aidha amesema Bunge linafanya taratibu za mazishi ya Mtema kwa mawasiliano na familia ya mbunge huyo na baadaye litatoa taarifa rasmi ya mazishi.
CHADEMA
Kwa upande wa CHADEMA katika taarifa yao kwa umma, imesema chama kimepatwa na majonzi makubwa na kinasikitika sana kwa kifo cha Mtema ambaye pia alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Taifa.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika (Mb) imesema Regia Mtema ambaye pia alikuwa Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira kambi rasmi ya upinzani bungeni.
Imesema katika uhai wake marehemu Mtema amefanya kazi mbalimbali za kisiasa na kijamii katika taifa. Marehemu Regia Mtema amezaliwa tarehe 21 mwezi Aprili mwaka 1980 na kusoma shule za sekondari kidato cha kwanza mpaka cha sita katika shule ya sekondari ya Forodhani na Shule ya Wasichana ya Sekondari ya Machame.
“Marehemu Mtema alipata shahada yake ya kwanza (Bsc Home Economics and Human Nutrition) katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine. Mara baada ya kuhitimu masomo yake marehemu Regia Mtema alifanya kazi katika taasisi mbalimbali kabla ya kujiunga na CHADEMA na kuteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Vijana ya CHADEMA na baadaye kuteuliwa kuwa Ofisa Mwandamizi katika Kurugenzi ya Mafunzo ya CHADEMA nafasi ambayo aliishikilia hadi mwaka 2010 alipoteuliwa kuwa mbunge wa viti maalum,” Imeeleza taarifa hiyo.
Mnyika amesema tayari viongozi wakuu wa CHADEMA wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Katibu Mkuu Dr. Wilbroad Slaa, wajumbe wa kamati kuu, wakurugenzi wa chama makao makuu na wabunge wameungana na familia ya marehemu katika kipindi hiki kigumu.
“CHADEMA inatoa pole kwa familia ya marehemu Regia Mtema, wanachama wote na wananchi wa Mkoa wa Morogoro hususani wa Jimbo la Kilombero kutokana na msiba huu wa ghafla katika wakati ambapo mchango wake ukihitajika kwa chama na kwa taifa.”
Amesema taarifa zaidi kuhusu taratibu za maziko, itatolewa mara baada ya kukamilisha majadiliano baina ya familia ya marehemu, chama na Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha mipango ya mazishi ya marehemu inapangwa nyumbani kwa Baba wa Marehemu Regia Mtema, Ndugu Estelatus Mtema, Tabata Chang’ombe. Ratiba ya maziko itatolewa baada ya kukamilika kwa taratibu zinazopangwa na familia ya marehemu, Ofisi ya Bunge na chama.
Mungu ailaze roho ya Marehemu Regia Mtema, mahali pema peponi. Amina.