Bunge lamng’ang’ania Jairo, launda tume kumchunguza umpya

Spika Anne Makinda akiwa na watendaji waendeshaji wa Bunge.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SIKU moja baada ya Katibu Mkuu Kiongozi Philemon Luhanjo kumrejesha kazini, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo mambo yamegeuka bungeni na sasa bunge limetamka kuunda tume ya kuchunguza zaidi tuhuma dhidi ya Jairo.

Alieanza kuonesha hali ya kutoridhika kwa hatua hiyo alikuwa ni Mbunge Kabwe Zitto wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, ambaye leo alisimama bungeni na kuomba utaratibu akitumia kanuni za bunge namba 51 na 55 (3). Katika hoja zake Zitto alisema; “Mheshimiwa Naibu Spika jana sote wabunge na Watanzania tumesikia taarifa ambayo Katibu Mkuu Kiongozi ameitoa kuhusiana na suala linalohusiana na Katibu Mkuu Nishati na Madini, David Jairo, na katika maelezo yake ameonesha kuwa tuhuma ambazo Mbunge Beatreace Shellukindo alizozitoa dhidi ya ndugu Jairo hazikuwa za kweli, yaani hazipo-lakini pili Katibu Mkuu Kiongozi akawa ameagiza kuwa Katibu Mkuu Nishati na Madini arejee Kazini leo,” alisema Zitto.

“Na Mheshimiwa Naibu Spika unafahamu kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizungumza ya kwamba ingekuwa yeye angekuwa tayari ameshamchukulia hatua ndugu Jairo na sitaki kusema kwamba Bunge linaweza likawa ni Mahakama, likaendesha kesi na kuhukumu, lakini kwa mujibu wa taratibu za mabunge ya Jumuiya ya Madola, kila muhimili una majukumu yake hasa ukizingatia kuwa katika maelezo ya Katibu Mkuu Kiongozi alisema kwamba ndugu Jairo anaweza akawashtaki wabunge kwa udhalilishaji,” alisema.

Pamoja na mambo mengine Zitto hakuridhishwa na kitendo cha taarifa hiyo kutolewa nje ya bunge tena ikiwa na majibu mepesi hivyo kuliomba bunge lisitishe shughuli za bunge hadi hapo taarifa hiyo juu ya uchunguzi wa tuhuma za Jairo itakaporejea bungeni ijadiliwe.

Hata hivyo hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi licha ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Uratibu (Bunge), William Lukuvi kusimama kutaka kuipinga hoja hiyo.
Baadaye Ndugai aliliarifu bunge kuwa hoja hiyo ni ngumu kuitolea uamuzi mwenyewe hivyo kuiomba Kamati ya Uongozi ya Bunge ikutane na kujadili jambo hilo kabla ya kurejeshwa tena bungeni.

Akitoa taarifa ya kikao hicho baadaye alisema kamati imepima uzito wa tatizo na kuridhiwa lijadiliwe bungeni hivyo Zitto kupewa nafasi ya kueleza kwa kina hoja yake, kabla ya wabunge wengine kuendelea. Mbunge mwingine aliyepata nafasi ya kuchangia hoja hiyo kwa uzito, alikuwa ni Mbunge wa Simnajiro, Christopher Ole Sendeka (CCM), ambaye baada ya kuchambua hoja hiyo alilishauri bunge kuundwa kwa tume ya kuchunguza tena jambo hilo ili kubaini ukweli wake kabla ya Bunge kutoa uamuzi.

Akihitimisha mjadala huo kwa kutoa mwongozo wake, Naibu Spika Ndugai amesema kikao cha Kamati ya Uongozi kilichokaa na kuongozwa na Spika Anne Makinda kimechagua majina ambayo yanaunda kamati itakayo chunguza kwa kina suala hilo upya kabla ya kutoa taarifa bungeni.