Bunge laipongeza Yanga kutwaa ubingwa wa Kagame

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeipongeza timu ya soka ya Yanga kwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame kwa kuwatandika watani zao timu ya soka ya Simba pia ya Dar es Salaam kwa gori 1-0.

Pongezi hizo zimetolewa bungeni jana na Spika wa Bunge, Anne Makinda muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu. Spika Makinda alisema bunge linaipongeza timu ya Yanga kwa ushindi wa huo na pia kuwezesha kombe hilo kubaki nchini.
“Kwa namna ya pekee kabisa, bunge linaipongeza timu ya soka ya Yanga kwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame, pia tunawapongeza Simba na Mashabiki wa timu zote mbili kwa utulivu wao,” alisema Spika Makinda.

Spika Makinda akiendelea kuzungumza alisema “hapa kuna tangazo kutoka kwa mheshimiwa mmoja anawakaribisha waheshimiwa wabunge, Ismail Rage, Samuel Sitta, Juma Nkamia, Musa Zungu, Job Ndugai, Kabwe Zitto, Prof. Juma Kapuya, Iddi Azzan, Willium Ngeleja na Khalifa Khalifa katika hafla ya kuipongeza timu ya Yanga.

…Lakini tangazo hili halijasema hafla hii itafanyika wapi, hivyo mlioalikwa mtajua mkiwasiliana na aliyeandika tangazo hili,” alisema Spika Makinda. Baada ya kusema hivyo Ukumbi wa Bunge ulilipuka kwa makofi kutoka kwa wabunge hali iliyoashiria lilikuwa ‘dongo’ kwa mashabiki wa timu ya Simba ambao ni wabunge.

Hata hivyo, alisema bunge linazipongeza timu za Yanga na Simba kwa kuingia fainali katika michuano hiyo, kwani zimeleta heshima kubwa kwa taifa kutokana na kulitwaa kombe hilo mara 10 ambapo Simba imelitwaa mara sita na Yanga mara nne.